The House of Favourite Newspapers

Kashfa ya Trilioni 1, JPM Amng’oa Waziri Lugola – Video

0

KASHFA ya mkataba wa kifisadi iliyomkumba Kangi Lugola, imesababisha kujiuzulu kwenye nafasi ya uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Lugola ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, amechukua hatua hiyo kufuatia kashfa ya wizara hiyo kuingia mkataba wenye utata wa thamani ya zaidi ya Sh. 1 trilioni na kukopa mkopo bila ruhusa ya Wizara ya Fedha na Mipango.

“Ninajua leo hapa Waziri wa Mambo ya Ndani haonekani hapa (alikuwepo), ameshaleta barua ya kujiuzulu na nimemkubalia, na nimempongeza kwa kutambua hilo.

“Lakini kitu kikubwa ni nini, ni watu kukosa uadilifu. Hivi karibuni kulikuwa na mkataba wa ajabu unatengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani, wenye thamani ya EURO milioni 408,” amesema Magufuli.

Amesema wizara hiyo imekosa uadilifu kwa kuwa ilidiriki kuingia mkataba wenye thamani ya Euro milioni 408, bila kupangwa katika bajeti na kupitishwa na Bunge.

“Umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Fire (Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji) na haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao, kuna kampuni moja nafikiri kutoka Romania, wahusika wanaokwenda kwenye majadiliano, wanalipwa allowance (posho), bado ya kulipiwa kwenye tiketi za ndege. Mradi wa ovyo wameusaini,” amesema Magufuli.

Akifafanua dosari za mkataba huo, amesema, masharti yake yanaibana serikali, pamoja na vifaa vilivyoorodheshwa katika mkataba huo ambavyo vinatarajiwa kununuliwa, havikidhi mahitaji ya nchi.

“Lakini commitment ya ndani inaeleza kwamba  ukitaka kuuvunja, yale yaliyoanza kutekelezwa, lazima yaendelee kutekelezwa. Mimi Lugola nampenda sana, ni mwanafunzi wangu pamoja na mwili wake mkubwa ni mwanafunzi wangu, lakini katika hili hapana.  Nilitegemea hata hapa nitamkuta hayupo, nasema kwa dhati,” amesisitiza rais kuongeza;

Licha ya Lugola kujiuzulu, vigogo wengine wa wizara hiyo waliong’oka kufuatia sakata hilo ni, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania, Thobias Andengenye.

“Kamishna Jenerali Andengenye nampenda sana, ni mchapakazi lakini kwenye hili hapana, nilitegemea hapa awe hayupo. Na ndiyo maana nampongeza Meja Jenerali Kingu aliyekuwa Katibu Wizara Mambo ya Ndani kwa kuwajibika.

Rais pia amesema, Wizara ya Mambo ya Ndani inaongoza kwa kumtesa, kwani inaongoza kwa kuwa na miradi pamoja na mikataba ya ovyo.

“Nimesema kazi ya uongozi saa nyingine ni ngumu, na tuna changamoto nyingi na hasa hii Wizara ya Mambo ya Ndani. Kama kuna wizara inanitesa, ni hii Wizara ya Mambo ya Ndani. nataka muelewe hivyo Watanzania, inatesa sana,” amesema na kuongeza kwamba katika miaka minne ya utawala wake, tayari tume nne zimeundwa kuchunguza baadhi ya mambo kwenye wizara hiyo.

Leave A Reply