Kasi ya Magufuli Inavyowatia Hofu Wavivu na Mafisadi

magufuli akimwaga sera katika viwanja vya mpilipili Lindi mjiniNi wazi kuwa hadi sasa Watanzania wengi watakuwa tayari wameshafahamu viongozi wapi watawachagua pindi itakapofika Oktoba 25 mwaka huu, hiyo ni kutokana na sifa na imani yao kwa viongozi hao.

Wengi bado wanaendelea kujipambanua kupitia kampeni wanazofanya kila siku, lakini ni jambo lililo wazi kuwa katika viongozi hao wapo wenye sifa nzuri za utumishi kutoka vyama mbalimbali na wengine wakiwa hawana sifa hizo lakini wote wanataka kupata madaraka hivyo lazima watumie kila mbinu kupigiwa kura na Watanzania.

Ukitazama vizuri utagundua kuwa wagombea hao ni wengi na wana maneno mazuri kiasi kwamba ni vigumu kusikiliza sera zao na kuzitofautisha. Hivyo basi kipimo rahisi kinachotumiwa na Watanzania wengi ni historia ya utumishi wa viongozi hao na pengine mvuto wa mtu husika katika umati wa watu.

Lakini wakati wagombea wengi wakidai kufanya mazuri ya kila namna kwa wananchi, mgombea mmoja tu ambaye ni Magufuli ameonekana kuwa wa kipekee kwa kuwa mkweli zaidi kwa kutozungumza mazuri tu bali hata ‘mabaya’ atakayowafanyia wale ambao hawataendana na kasi yake ya maendeleo, jambo ambalo katika jamii ya Tanzania yenye wababaishaji wengi maana yake ameongeza kundi kubwa la watu watakaompiga vita kwa kuwa tu ametangaza kuwawajibisha pindi atakapoingia ikulu.

Sikatai kuwa wapo wagombea wengine ambao pia wamesema hivyo lakini hawahofiwi sana kuliko Magufuli ambaye ameyagusa makundi yenye nguvu kubwa nchini.

Ni wazi kuwa Magufuli ndiye mgombea anayekubalika na kila mtu kwa uchapakazi wake lakini watu hao wapo wanaomkubali ingawa wanakichukia chama chake kwa kauli kuwa Magufuli ni msafi na anafaa kuwa rais isipokuwa chama chake ndicho tatizo.

Kwa hoja hiyo utaona kabisa kwamba watu hao wapo radhi kutupa kura yao kwa kiongozi yeyote wa chama kingine bila kujali ana maadili ya uongozi au la jambo ambalo ni baya kwa taifa letu kwa miaka mitano ya utumishi wa hao watu  kama tu watashinda.

Kauli za Magufuli ambazo ukiangalia kwa jicho la tatu ndiyo zinaweza zikawa zinamharibia, lakini ndizo hasa zinazonifanya nimuone kama kiongozi shujaa ni zile alizozizungumzia katika kampeni zake kuwa atashughulika nazo kama ilani yake pindi akiwa rais.

Kwanza ni suala la mafisadi, ambapo bila kujali anazungukwa na CCM wenzake wanaotuhumiwa sana kuwachekea mafisadi, lakini yeye alisimama kidete na kudai kuwa akiingia madarakani ataunda mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi ambao mwenyewe alidai kuwa wameifikisha nchi katika hali ya umasikini wakati nchi hii ni tajiri. Hapa baadhi ya watu wenye mtazamo mmoja huweka hoja kuwa CCM ndiyo yenye mafisadi pekee bila kufikiri kuwa wapo mafisadi wengi ambao ni wafanyabiashara wakubwa wasiofungamana na chama chochote na mafisadi wengine wakiwa viongozi wa vyama pinzani.

Pili ni suala la kuwashughulikia watumishi wa umma wavivu ambao wanarudisha gurudumu la maendeleo nyuma na hatimaye kuiangusha serikali kwa ujumla kwa kuwa na watendaji wavivu.

Hapo aliwazungumzia walimu, wafanyakazi wa maofisini, watendaji wa kata na mitaa, madaktari na makundi mengi mengine ambayo kiuhakika makundi hayo yana nguvu sana katika jamii.

Kwa maneno hayo ni wazi kuwa Magufuli amejitangazia vita na mafisadi na watumishi wavivu ambao ndiyo wanaongoza kwa kumpiga vita hivi sasa kwa kuwa uoga wao unaongozwa na hofu ya wao kung’olewa madarakani na kufunguliwa mashtaka.

Sasa nastaajabu kuwa kama kiongozi wa kariba hiyo tutamwacha kwa kushawishiwa na watu ambao kiasili ni watendaji wabovu na mafisadi maendeleo tutayapata kupitia  rais gani?


Loading...

Toa comment