The House of Favourite Newspapers

Kassim Kayira: Kutoka mkimbizi, babantilie, BBC hadi Azam TV

0

kassim kayiraNI lazima uwe na watu ambao unataka kuwa kama wao. Hayo ndiyo maisha. Kujua njia walizopitia hadi kufika mahali unapopatamani ni moja ya ngazi muhimu sana kukusogeza katika maisha hayo.

Kassim Kayira, kama anavyojulikana katika ulimwengu wa habari kuwa ni miongoni mwa waandishi nguli kabisa wa kimataifa, anasimulia safari yake ya maisha tangu kuzaliwa hadi kufikia mafanikio aliyonayo katika habari.

Hii ni sehemu ya tano, akisimulia hatua kwa hatua. Wiki iliyopita, tuliishia pale wakati wa mazungumzo yakiwa yamekolea, ghafla namuona Kayira akiinuka na kuniambia jambo ambalo linanifanya nikose raha ghafla.Je, ni lipi hilo?
SHUKA NAYO SASA…

“Aise, hebu ngoja kwanza nimuone bosi huko ofisini, maana wakati ule alikuwa na wageni lakini alinitaka niwe namuangalia mara kwa mara, sidhani kama leo tutamalizia mahojiano haya na kama nilivyokueleza, kuwa kesho natakiwa kusafiri kwenda nchini Uganda, ngoja tuone,” anasema Kayira akiwa ameshikilia kitasa cha mlango cha chumba hicho, tayari kwa kuondoka huku akinitaka nimsubiri.

“Oke, hakuna shida,” namjibu kwa sauti ya unyonge.
Hata hivyo, dakika tatu au nne baadaye, ghafla mlango wa chumba hicho unafunguliwa na Kassim anaingia kwa kasi kama aliyekuwa akifukuzwa.

“Sasa, inabidi twende kule Tazara kuna mzigo nataka nikachukue huko, lakini mazungumzo yaendelee ndani ya gari, tayari nimeshapewa dereva wa kunipeleka,” anasema Kayira na kulivaa vyema begi lake mgongoni, tunatoka nje na kupanda gari maalum lililokuwa na nembo nyingi za Azam TV.

“Mmmh, ikawaje kaka?,” naamuuliza ili aendelee na simulizi yake.
“Basi bwana, kazi ikazidi kunoga, nikiwa bosi mkubwa kabisa pale TV Rwanda, lakini sikuridhika na hapo kabisa, nikazidi kuwa mbunifu, lakini wakati hayo yakiendelea, umaarufu nao ukashika kasi,” anasema Kayira na kuachia tabasamu la kiaina.

“Mwaka 1998, nilienda nchini Zambia kwa masomo maalum katika Chuo cha Thomson Foundation, ambako nilisoma Kiingereza na Kozi ya Utawala katika Utangazaji (Broadcasting Management).

“Baada ya hapo, nikafanya kazi kidogo, lakini nikaenda nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Wales kuchukua masomo ya juu na niliporudi nchini Rwanda, tayari nikawa mhariri mkuu wa habari katika Televisheni ya taifa,” anasema Kayira.

“Lakini du, hapa acha niseme jambo moja, wanawake wa Rwanda wana majaribu sana aisee, unajua duniani kote, hakuna wanawake wazuri kwa maana ya maumbo kama Wanyarwanda, kilichonisaidia ni kuwa tayari nilikuwa nimeshaoa na pia mimi ni mtu wa dini sana.

“Lakini aaah, yalikuwa ni majaribu makubwa, maana nilikuwa katika kiwango changu cha juu cha umaarufu, aah, Rwanda, wewe acha tu ni kwa vile maisha hayawezi kurudisha siku za nyuma,” anasema Kayira.

“Kufikia hapo, nikateuliwa kuwa natembea na rais kwenye ziara zake, kwa kweli nilizunguka sana na Rais Kagame, nimetembea nchi nyingi nikiwa na rais kama mwandishi wa habari wa Televisheni ya taifa,” anasema Kayira.

“Nini umejifunza na kufaidika katika ziara za rais?” namuuliza lakini badala ya kujibu swali langu, Kayira anaingiza kitu cha tofauti kidogo.

“Unajua nafurahia sana uwepo wako na mimi kwa leo,” anasema kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kiganda.

“Kwa nini?” namuuliza na kumtazama usoni.
“Mimi nimefanya mahojiano na watu wengi sana duniani, lakini pia nimefanyiwa mahojiano na waandishi kadhaa, lakini naona una kitu cha ziada,” anasema Kayira na kutabasamu.

“Mmh, hebu jibu swali langu la awali,” naishia.
“Oke, faida ni nyingi sana, marupurupu mengi, kujua maisha binafsi ya rais na mambo mengine mengi zaidi,” anasema Kayira.
“Kujua maisha binafsi ya rais, kivipi?” namuuliza kwa shauku ya kutaka kujua maana halisi ya sentensi hiyo.

“Aaah, unajua rais anapokuwa ziarani, anakuwa yeye kama yeye, japo nafasi na hadhi yake kama rais viko palepale lakini yanakuwa ni maisha ya kibinafsi zaidi,” anasema Kayira.

“Sijaelewa, fafanua zaidi kaka,” namuuliza tena, safari hii naacha kuandika ili nimsikilize kwa makini zaidi.

“Yaani rais anakuwa akijiachia zaidi kwa maisha binafsi, mnakuwa na mazungumzo ya kawaida na rais kama washkaji, mnakula pamoja, mnataniana kidogo, yaani mnapata nafasi ya kumjua rais zaidi ya nafasi aliyonayo,” anajitahidi kufafanua Kayira.

Je, nini kitafuata? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply