The House of Favourite Newspapers

Kasuku Afanyiwa Upasuaji Kichwani

 

MADAKTARI wa wanyama nchini New Zealand wamemfanyia upasuaji kasuku mmoja kutoka jamii ya kakapos ambayo ipo hatarini kutoweka.

 

Madaktari hao wa upasuaji, walitumia mbinu za upasuaji zinazotumika kwa binadamu na wanyama wengine jamii ya mamalia kumfanyia upasuaji kifaranga hicho cha kasuku chenye siku 56. Kifaranga hicho kilikuwa na tundu kwenye fuvu.

 

Kakapos – ndiyo kasuku wanene zaidi duniani – hawapai na hutoka usiku tu. Hata hivyo, aina hiyo ya kasuku ipo hatarini kutoweka kutokana na kuwindwa na majangili na wanyama wengine wa mwituni.

 

Kwa sasa kuna kasuku jamii ya kakapos 144 tu duniani, na wanapatikana katika visiwa vya New Zealand. Kifaranga hicho kilichopewa jina la Espy 1B, kilitotolewa katika kisiwa cha Codfish kusini mwa New Zealand na kipo chini ya uangalizi wa Idara ya Uhifadhi ya Wanyama ya kisiwa hicho, na wafanyakazi wa kitengo hicho ndiyo waligundua uvimbe kichwani mwake.

 

 

Kifaranga hicho kilisafirishwa na shirika la ndege la nchi hiyo mpaka kwenye hospitali ya wanyama ya Wildbase ya Chuo Kikuu cha Massey ambapo upasuaji huo ulifanyika.

 

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa hospitali hiyo, Profesa Brett Gartrell, imesema kulikuwa na ngozi nyembamba iliyotenganisha ubongo wa kifaranga hicho na dunia.

 

“Shimo hilo liliruhusu sehemu ya ubongo kutokeza na kusababisha uvimbe.” amesema profesa huyo na kuongeza kwamba upasuaji huo hatari wa ubongo ulibidi ufanyike ili kunusuru maisha ya ndege huyo, lakini pia alikiri kuwa: “Kitu kama hicho hakijawahi kufanyika kwenye historia ya matibabu ya ndege.”

 

 

Maofisa wa hospitali ya Wildbase wanasema upasuaji huo uliofanyika wiki iliyopita umefanikiwa na kifaranga hicho kinaendelea vizuri.

 

Kasuku wa jamii ya kakapos walikuwa ni moja ya jamii kubwa ya ndege nchini New Zealand, lakini sasa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Maliasaili (IUCN) limeiweka jamii hiyo ya kasuku kama wanyama ambao wamo hatarini kuangamia. Hivi karibuni, jamii hiyo ya kasuku iliweza kupata msimu bora zaidi wa kuzaliana katika miaka ya hivi karibuni.

Comments are closed.