Katikati Ya Msimu, Barcelona Haijawahi Kufukuza Kocha Tangu 2003

UKISIKIA kuchezea sharubu ndiyo hivi sasa. Kocha Ernesto Valverde ni kama anachezea sharubu za waajiri wake Barcelona akionekana kama vile anawalazimisha wafanye kitu ambacho hawajawahi kukifanya tangu mwaka 2003.

 

Matokeo mabaya ambayo Valverde anaendelea kuyapata, ni kama kuchezea sharubu za waajiri wake.

Barcelona haina uhakika wa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) msimu huu, ikiwa inafukuzana na Real Madrid, Atletico Madrid na Sevilla kileleni.

 

Tayari imeshapoteza mechi tatu na sare nne kwenye michuano hiyo lakini juzi ilitupwa nje ya michuano ya Supercpa de Espana kwa kuchapwa 3-2 dhidi ya Atletico Madrid.

 

Barcelona hawajawahi kufukuza kocha katikati ya msimu tangu mwaka 2003. Imepita miaka 17 sasa. Lakini mwendo wa Valverde unaonekana kuwala zimisha kufanya kitu ambacho hawajawahi kufanya kwa miaka mingi.

 

Kwa miaka yote hiyo tangu 2003, kocha wa Barcelona ni lazima amekuwa akimaliza msimu na kuondoka zake kwa amani.

 

Sasa mashabiki wa Barcelona, wakurugenzi na watu wote wa karibu na klabu hiyo, wanapita katika hisia kali ambazo zimekuwa hazipo kichwani mwao kwa muda mrefu.

Kwa sasa kuna mawazo ya kufukuza kocha katikati ya msimu, suala ambalo hawajawahi kulifanya kwa miaka 17.

 

Wakiwa wamepita makocha watano, mechi 145 na miaka 17, Valverde anakaribia kuondoshwa kwa fedheha na kuingia katika historia mbaya Barcelona.

Tazama msimu wa 2002/03 ambao ndio ulikuwa wa mwisho kwa Barcelona kufukuza kocha katikati ya msimu.

 

Ilikuwa ni Januari 26, 2003. Barcelona ilichapwa 2-0 na Celta Vigo ikaporomoka hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa La Liga, hapo ikabidi kocha Louis van Gaal aonyeshwe mlango wa kutokea, nafasi yake ikachukuliwa na Antonio de la Cruz, kisha baadaye Radomir Antic akachukua mikoba hadi mwishoni mwa msimu katika kipindi cha mpito kabla ya kutua kwa Frank Rijkaard.

 

Rijkaard alitwaa taji lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006 ukiwa pia ni ubingwa wa pili kihistoria kwa Barcelona katika michuano hiyo baada ya kushinda kwenye fainali dhidi ya Arsenal jijini Paris.

 

Rijkaard aliiongoza Barcelona kwa miaka mitano kuanzia 2003 hadi 2008 alipompisha Pep Guardiola.

Guardiola anatazamwa na wengi kama mmoja wa makocha bora katika historia ya Barcelona. Bosi huyu wa sasa wa Manchester City alikuwa na misimu minne ya mafanikio Camp Nou. Akitwaa mataji kibao na kuwa na moja ya misimu bora zaidi katika soka.

 

Hata hivyo, kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho, Guardiola aliondoka mwishoni mwa msimu wa 2011/12 na mikoba yake akamuachia Tito Vilanova.

Msimu wa 2012/13 ulikuwa ni moja ya misimu yenye changamoto kwa Barcelona kutokana na maradhi makubwa ya kocha wao Tito Vilanova.

 

Licha ya kuuguaugua karibu kwa msimu mzima, Vilanova aliipa Barcelona ubingwa wa La Liga na mwishoni mwa msimu akajiuzulu kisha akafariki dunia mwaka mmoja baadaye, yaani Aprili 25, 2014 kwa ugonjwa wa kansa.

 

Msimu uliofuata, Barcelona ilikuwa na kocha mwingine Tata Martino naye akaiongoza kwa msimu mmoja, ingawa angeendelea angefukuzwa kwa kuwa staili yake ya soka na mbinu zake hazikupendwa na viongozi wa klabu hiyo pamoja na mashabiki.

 

Chini ya Luis Enrique, Barcelona iliweka historia msimu wa 2014/15 ambapo klabu hiyo ilishinda ‘treble’, yaani makombe matatu makubwa. Huyu aliiongoza Barcelona hadi 2017.

 

Alipoondoka, ndiyo Valverde akatua kwa ajili ya msimu wa 2017/18 lakini baada ya vipigo vya kukumbukwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Roma kwenye Uwanja wa Olimpico halafu msimu uliopita kufungwa na Liverpool Anfield, inaonekana kama ana nafasi kubwa ya kupoteza nafasi yake kama kocha.

 

Na sasa matokeo ya Barcelona yamekuwa ya kupanda na kushuka. Je, klabu hiyo itaweka rekodi mpya kwa kufukuza kocha katikati ya msimu?

 

MAFANIKIO YA MAKOCHA

BARCELONA TANGU 2003

  1. VAN GAAL

La Liga: 1997–98, 1998–99

Copa del Rey: 1997–98

UEFA Super Cup: 1997

  1. RIJKAARD

La Liga: 2004–05, 2005–06

Supercopa de España: 2005, 2006

UEFA Champions League: 2005–06

  1. GUARDIOLA

La Liga: 2008–09, 2009–10, 2010–11

Copa del Rey: 2008–09, 2011–12

Supercopa de España: 2009, 2010, 2011

UEFA Champions League: 2008–09, 2010–11

UEFA Super Cup: 2009, 2011

FIFA Club World Cup: 2009, 2011

  1. VILANOVA

La Liga: 2012–13

  1. MARTINO

Supercopa de España: 2013

  1. ENRIQUE

La Liga: 2014–15, 2015–16[94]

Copa del Rey: 2014–15, 2015–16, 2016–17

Supercopa de España: 2016

UEFA Champions League: 2014–15[94]

UEFA Super Cup: 2015

FIFA Club World Cup: 2015

  1.  VALVERDE

La Liga: 2017–18, 2018–19

Copa del Rey: 2017–18

Supercopa de España: 2018

 

BARCELONA, Hispania

Toa comment