The House of Favourite Newspapers
gunners X

Kato Alipojipachika Ubosi…

0

 

Na Ben Kato

KATO kijana wa mjini aliyetekwa na starehe lakini zaidi akihusudu pombe, anakutana na visa mbalimbali katika maisha yake ya kila siku.

 

Kila kukicha, Kato anafungua ukurasa mpya wa vituko. Leo anafanya hiki, kesho anafanya vile.

 

Katika safu hii ya kila JUMAMOSI Kato ataonekana na vituko vyake hivyo ambavyo kwa hakika vitaifanya wikiendi yako kuwa nzuri na ya kupendeza.

 

Andaa mbavu zako kupambana na VITUKO VYA KATO. Mbunifu wa visa hivi ni BEN KATO. Fuatana naye leo na kila Jumamosi, lakini leo tunakupa kionjo cha kufungulia wiki, ila utakutana na Kato kila JUMAMOSI.

…………………………………………….

 

 

KATO amefanikiwa kupata kazi ya maana kidogo. Mshahara wake unamruhusu kufanya jeuri mjini. Siku ya kwanza tu kutoka kazini, akaamua kuingia katika baa moja iliyokuwa karibu ofisini ili kukwepa foleni.

 

Akafika katika meza iliyopo mwishoni kabisa mwa baa hiyo. Akaagiza ulabu wake. Kabla mambo hayajaanza kukolea akavutiwa na mrembo mmoja mwenye umbo namba nane.

 

Akaamua kujisogeza katika meza hiyo na kuanza kumwangalia kwa kuibia, huku udenda wa mahaba ukimtoka.

Akaona isiwe tabu, akamsogelea…

 

KATO: Dada samahani naweza kujumuika na wewe?

DADA: Aaaahmhh anyway It’s okay, karibu.

 

KATO: Naitwa Kato, ni bosi mwandamizi katika kampuni moja hapa mjini. Ofisi zetu zipo jirani sana na hapa.

DADA: Oooh! Nashukuru sana kukufahamu. Mimi naitwa Scola.

 

KATO: Dooooh! Jina zuri sana.

 

Stori za hapa na pale zikaendelea, Kato akaanza kumsogelea Scola na wakati mwingine kuanza kumshikashika. Hakujali chochote maana alikuwa amelewa.

 

Dakika chache baadaye akashangaa kumuona bosi wake akitokea, akaelekea kwenye meza aliyokuwa amekaa na Scola.

 

BOSI: Kato unafanya nini na mke wangu hapa? Halafu nimekufuatilia muda mrefu sana, naona unamshikashika. Ni adabu gani hii?

KATO: Si…si…sikujua bosi…u…u…unajua…

BOSI: Sitaki ngonjera zako Kato. Umenikosea adabu sana, hivyo basi kuanzia sasa hivi sitaki kukuona ofisini tena.

 

KATO: Mkuu tafadhali…

BOSI: Nimemaliza, huna kazi na huna malipo yoyote, potea.

 

SCOLA: We’ kaka si ulisema wewe ndiyo bosi? Imekuwaje tena?

Kato hakujibu zaidi ya kuondoka kwa aibu.

Kazi ya Kato ikaota majani.

Leave A Reply