Katumbi aweka Sh bil 5 kwa Samatta

SamataBwana580211.jpgIbrahim Mussa na Hans Mloli

MBWANA Samatta anaelekea kuweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji wa Tanzania mwenye thamani kubwa zaidi kwani Bosi wa TP Mazembe, Moise Katumbi ameitangazia Koninklijke Racing Club Genk ya Ubelgiji dau la euro milioni 2.5.

Kwa thamani ya sasa ya fedha, euro milioni 2.5 ni sawa na Sh bilioni 5.7, hivyo kama dili likikaa sawa Samatta ambaye ni straika wa zamani wa Simba atakuwa mchezaji ghali zaidi raia wa Tanzania.

Chanzo chetu makini kutoka ndani ya Klabu ya Genk, kimethibitishia kuwa, Katumbi amekubali kumuuza Samatta kwao kwa dau la euro milioni 2.5 na sasa mazungumzo yanaendelea kati yao.

“Katumbi anataka euro milioni 2.5 na tayari wawakilishi wetu wameshaambiwa na wapo katika vikao ili kufikia uamuzi sahihi.

 “Katumbi alikuja hapa Ubelgiji kwa ajili ya mazungumzo na kama dili litakamilika basi Samatta atajiunga nasi ifikapo Januari mwakani.”

“Baada ya Katumbi kutaja dau lake, na sisi tumepa ofa yetu ambayo ni pungufu kutoka katika fedha aliyoitaja, alikutana na mwanasheria wake hapa Ubelgiji na kututaka tutoe ofa nyingine ya juu zaidi.

“Hivi sasa tunajipanga kutoa ofa nyingine kwao kwani sisi tunamtaka Samatta ili tuweze kumtumia katika mechi zetu za ligi na michuano mingine. Hadi tunatoa ofa ya kwanza mwenyewe Katumbi alikuwepo hapa lakini sasa ameondoka ila mwanasheria wake ndiye amebaki.

 “Tangu Alhamisi (juzi) vikao bado vinaendelea juu ya kulimaliza suala hili lakini leo (jana Ijumaa) na kesho (leo) hatutaweza kukaa kama timu kuzungumzia ofa nyingine kwani tupo katika mapumziko ya Krismasi.

“Nadhani kuanzia Jumatatu (keshokutwa) tunaweza kukutana na kuzungumzia ofa mpya halafu tutaiwakilisha kwa mwanasheria wa Mazembe ambaye amebaki hapa Ubelgiji,” kilisema chanzo hicho.

Taarifa zaidi zinasema, Katumbi sasa anapambana kuhakikisha anamuuza Samatta kwa wakati huu kwani ndiyo muda wake wa kupata faida kwa kuwa ikifika Aprili mwakani ataondoka bure kwani atakuwa amemaliza mkataba.

“Kuna njia mbili tu za Samatta kutua Genk endapo ofa yetu itakataliwa tena na Katumbi, kwanza tunaweza kumsubiri hadi atakapomaliza mkataba wake au tutamshauri aununue mkataba wake na Mazembe.

“Unajua thamani ya mchezaji huwa na utata endapo anaelekea kumaliza mkataba wake halafu akiwa katika ubora kama wa Samatta, sisi tupo makini na hilo,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Genk.

Genk inayofundishwa na Kocha Peter Maes, inasifika kwa kuzalisha wachezaji nyota kadhaa wakiwemo Thibaut Courtois na Kevin De Bruyne walitoka hapo na kwenda Chelsea japokuwa De Bruyne sasa yupo Manchester City.

Pia Genk ilimuuza Christian Benteke (sasa yupo Liverpool) kwenda Aston Villa mwaka 2012 kwa dau la euro milioni 10. Ilipowauza Courtois na De Bruyne pia mwaka 2012, Genk ilipata faida ya euro milioni 28.

Kama dili likienda sawa, kuna uwezekano mkubwa wa Samatta kuichezea timu hiyo inayotumia Uwanja wa Cristal Arena unaoingiza mashabiki 15,000 uliopo jijini Genk kisha kuuzwa Ulaya hata England haraka kama De Bruyne, Benteke na Courtois endapo atafanya vizuri.

Genk tangu kuanzishwa kwake mwaka 1988, imewahi kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne na Kombe la Europa mara tatu ambapo msimu uliopita ilifika hatua ya makundi.

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Samatta, wawakilishi wa straika huyo hawataki mchezaji huyo aondoke Mazembe kwa uhasama hivyo wanajitahidi kuweka mambo sawa ili aondoke kwa amani katika klabu hiyo.


Loading...

Toa comment