The House of Favourite Newspapers

Kauli Za Ovyo Za Manara Haziendani Na Matokeo Ya Ovyo Ya Simba

Haji Manara ambaye ni Ofisa Habari wa Simba.

MOJA kati ya vitu ambavyo vinachangia mchezo wa soka kuingiza fedha kwenye baadhi ya nchi au baadhi ya maeneo ni jinsi gani wahusika wanaweza kuutumia kutengeneza soko la kuufanya mchezo huo kuwa biashara.

 

Kwa miaka mingi Tanzania tumekuwa tukilia kuhusu viongozi kutokuwa na mfumo mzuri wa kuzifanya Simba na Yanga kutengeneza fedha ili ziendane na ukubwa wa majina ya klabu hizo.

Kiuhalisia huo ni wimbo wa miaka nenda rudi, lakini kwa sasa ni kama dunia sasa imeanza kuelekea kule ambapo wapenda soka wengi wamekuwa wakipata, yaani kuufanya mchezo wa soka kuwa biashara.

 

Siyo kwamba hakukuwa na biashara miaka iliyopita bali ni mifumo mibovu ambayo ilitengeneza watu wachache kuingiza fedha wao binafsi badala ya taasisi.

 

Kwa hilo naipongeza Simba kwa kuwa imeanza kuonyesha njia, kwani kwa muda mrefu mtaji wa mashabiki wengi katika vigogo hao umekuwa ukitumiwa vibaya. Kuelekea katika mabadiliko hayo, mtu kama Haji Manara ambaye ni Ofisa Habari wa Simba amekuwa akifanya kazi nzuri, ingekuwa kwenye siasa ningesema ni mtu sahihi kwenye kitengo cha ‘propaganda’.

 

Ndiyo ni propaganda hasa, ni mtu sahihi kwenye nafasi hiyo na amefanya mengi mazuri, hata kama kulikuwa na makosa huko nyuma ni ya kibinaadamu, lakini kihalisia Manara amekuwa na ushawishi mkubwa na kufanya mashabiki wa soka wa timu zote kuitazama Simba kwa jicho tofauti.

 

Madoido, propaganda ni muhimu sana wakati mwingine katika kuitengeneza brandi, ndiyo maana unaweza kukuta wachezaji walewale wa timu ya Mbeya City wakivalishwa jezi ya timu hiyo wanaweza kuwa na matokeo ya kawaida lakini wakivalishwa jezi ya Simba au Yanga, unaweza kuona mabadiliko yao.

 

Huo ni mfano mwepesi wa kutambua ukubwa wa brandi ya kitu Fulani, Simba ni kubwa lakini maneno ya Manara yamekuwa na msaada mkubwa miaka ya hivi karibuni katika kuongeza chachu ya kuifanya Simba iwe inatazamwa tofauti hasa ndani ya Tanzania.

 

Pamoja na pongezi hizo, hivi karibuni Manara alikuwa na shughuli yake binafsi na katika mkutano wake na waandishi wa habari (wa binafsi), akatumia nafasi hiyo kuizungumzia Simba.

 

Katika mkutano huo aliwzungumzia wale ambao wamekuwa wakimtukana na kupinga harakati zake za kuzindua biashara yake na taasisi yake binafsi huku Simba ikiwa imefungwa, alikuwa na hoja kwa kuwa Manara hawezi kuendelea kubaki klabuni hapo maisha yake yote.

 

Matusi au lugha kali ni kweli hazifai lakini kwenye soka la Tanzania ni kitu cha kawaida, lakini kwa aina ya uwasilishaji wake, Manara alionyesha kuwa mwenye hasira na sehemu ya maelezo yake aliwaita wale wanaopinga alichokifanya kuwa ni ‘wapumbavu’.

 

Nani ambaye hajui Manara ni mfalme wa mbwembwe hasa Simba inapokuwa inafanya vizuri, sasa hao waliokuwa wanampinga kufanya shughuli yake binafsi ni ndani ya klabu au watu wa nje? Kweli maoni ya mashabiki wa Instagrama ndiyo uwende ukawajibu kwenye mkutano makini wa kibiashara kama ule kwa kuwaaambia ni wapumbavu! Inashangaza sana, labda anatafuta mlango wa kutokea.

 

Kwa maelezo ya Manara nimebaini kuna mambo mawili hapo, kwanza, alifanya makusudi akijua biashara ya wadhamini wake iliyopo nyuma kwenye mabango itaonekana kwa sana, pili kuna kitu kinafukuta ndani ya klabu akaona hiyo ndiyo njia ya kutolea lile lililo moyoni mwake kwa njia anayoijua yeye.

 

Kama amekubali kuwa kuwa kioo cha jamii, anatakiwa kukubali dhihaka za mashabiki ni kitu cha kawaida. Niliona ametumia ukurasa wake akisema kuwa aliwalenga wale waliomtukana mzazi wake, lakini nilipotazama mkutano wake ule zaidi ya mara tano, kauli za hasira alizotoa nyingi zilikuwa zinamuhusu yeye kushambuliwa kwa lugha kali

Comments are closed.