The House of Favourite Newspapers

Kaze Aanika Siri ya Metacha Kuokoa Penati ya Namungo

0

 

KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, ndiye sababu kubwa ya kipa wa kikosi hicho, Metacha Mnata, kucheza penalti ya Bigirimana Blaise wakati timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili iliyopita, imefahamika.

 

Kabla ya penalti hiyo kupigwa, Metacha alipewa maelekezo kuwa Blaise hupiga penalti zake upande wa kulia, hivyo kutakiwa kufuata mpira upande huo atakapopiga, hivyo kufanikiwa kuicheza.

 

Kipa huyo alionekana kupata maelekezo kutoka kwa Kaze kabla haijapigwa na baada ya hapo akaonekana kuwahamasisha mashabiki wa Yanga kuanza kushangilia na kisha kufanya kile alichoagizwa kukifanya.

 

Baada ya mechi kumalizika kwenye Uwanja wa Mkapa, Kaze aliwapa kazi waandishi wa habari wakaangalie mechi kati ya Namungo dhidi ya JKT Tanzania watagundua siri ya kwa nini kipa wake aliokoa penalti hiyo.

 

“Niwape siri? Nendeni mkaangalie mechi ambayo Namungo walicheza na JKT Tanzania, mtajua ni kwa nini nilimpa maelekezo kipa wangu kitu cha kufanya,” alisema kwa kifupi.

 

Ukiiangalia mechi iliyochezwa Novemba 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Lindi, Blaise alipiga penalti yake upande wa kulia na kumfunga kipa wa JKT Tanzania, akiisawazishia timu yake bao, mechi iliyoisha kwa sare ya bao 2-2.

 

Kilichotokea Lindi ndicho kilichoonekana kutokea Dar es Salaam juzi, kasoro ilikuwa ni kwamba mechi dhidi ya JKT Tanzania mpira uliingia wavuni.

 

Jinsi Metacha alivyoonekana kusogea upande wa kulia mara moja kabla hata Blaise hajapiga na kweli mpira ukapigwa upande huo huo, hivyo kutopata ugumu wa kuruka sana, ilionyesha kocha huyo alimwambia kuwa Blaise hupiga penalti zake upande wa kulia. Ikumbukwe kuwa Kaze na Blaise wote ni raia wa Burundi, hivyo anamjuana vema kisoka.

Leave A Reply