Kaze Awafanyia Sapraiz Simba kwa Mkapa

LEO Jumamosi kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa pale Uwanja wa Mkapa, Dar huenda mashabiki wa Simba wakakutana na sapraiz kutoka kwa wapinzani wao Yanga.

 

Sapraiz hiyo ambayo watakutana nayo ni kocha Cedric Kaze kuwepo kwenye benchi la ufundi la Yanga kwa ajili ya kusaidiana na kocha Nassredine Nabi kwa ajili ya kusaka ushindi.

 

Kaze ambaye alitua nchini usiku wa kuamkia juzi akitokea Canada kwa ajili ya kuja kuchukua majukumu ya ukocha msaidizi ndani ya timu hiyo baada ya kuondolewa katika ya msimu uliopita alipokuwa kocha mkuu.

 

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa kocha huyo leo Jumamosi atatarajiwa kuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo katika mchezo huo dhidi ya Simba.

 

Jana mchana Yanga walimtambulisha kocha huyo kwa kumpa jezi ya timu hiyo akiwa sambamba na Mwinyi Zahera ambaye ni Mkurugenzi wa soka la vijana. Championi lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Dominick Albinus ambapo alisema:

 

“Kuhusu ishu ya kumpa mkataba Kaze au kutompa tutatoa majibu baada ya vikao vyetu ambavyo tumefanya jana (juzi Alhamisi) na leo (jana) Ijumaa ila mpaka sasa suala hilo hatujaanza kulijadili.”

 

“Kikao hicho tumefanya maalum kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi ambao tutacheza dhidi ya Simba pia tutakuwa na mada zingine hivyo baada ya kikao hicho nitakupa mrejesho wa kila kitu,” alisema Albinus.

IBRAHIM MUSSA NA LEEN ESSAU, Dar es Salaam


Toa comment