Kazi Ipo Dar Live Kesho!

Twanga (2)Twanga

UNAJUA kwa nini Hassan Rehani Bitchuka mwimbaji mahiri wa Mlimani Park Ochestra wana Sikinde anaitwa ‘Super Sterio’? Shaaban Dede na Msondo Music Band wana ukali gani katika Muziki wa Dansi siku hizi? Twanga na Ally Choki wako vipi? Wote hawa ni moto wa kuotea mbali na watakuwa jukwaa moja Dar Live, Mbagala Zakhem, kesho.

Twanga (1)Choki

Meneja wa Ukumbi wa Dar Live, Juma Mbizo alisema majibu hayo yatapatikana usiku wa kesho wakati bendi hizo zitakapooneshana umahiri wakishirikiana na ‘vijana wao’ The African Stars ‘Twanga Pepeta’ katika onesho maalum la Valentine’s Day. Nyimbo zao zote zilizovuma zamani zitapigwa ‘laivu’ leo katika onesho hilo ambalo kiingilio chake ni Sh. 10,000 kwa viti vya kawaida na Sh. 20,000 kwa V.I.P.

msondoMsondo

Nyimbo kama Hiba, Fikiri Nisamehe, Barua Kutoka Kwa Mama, Neema na kadhalika za Sikinde zitapigwa leo. Msondo Ngoma nao licha ya Dede, imesheheni mwanamuziki mahiri kama vile Roman Mng’ande ‘Romario, Salehe Bangwe, bila kuwasahau Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera mpiga solo mahiri ambaye tangu ajiunge katika bendi hiyo hajathubutu ‘kuikimbia.’

Baadhi ya nyimbo ‘zilizogongwa’ na bendi hii na ambazo zitapigwa leo Dar Live ni pamoja na Kicheko, Mawifi Mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama Katika Dimbwi, Mti Mkavu na Mizimu. Mbizo amethibitisha kuwa nyimbo nyingine ni Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la Mlemavu, Piga Ua Talaka Utatoa, Tuma, Wapambe, Asha Mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya Kusikitisha, Mwana Mkiwa, Kalunde, Kaza Moyo, Jesca, Kwenye Penzi, Binti Maringo, Dalili na nyingine nyingi.

Kwenye safu ya uimbaji Dede atasaidiana na akina Juma Katundu, Twaha Mohamed, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo. Kiongozi wao Saidi Mabera ataongoza safu ya wapiga magitaa ya solo na rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’.

Kwa upande wa gita zito la besi wapo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’ na drums huchanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe. Tarumbeta zitapulizwa na kijana machachari Roman Mng’ande na Hamis Mnyupe. Dorice George atapiga Tumba, Drums akisaidiwa na Amiri Said Dongo.

Naye Kiongozi wa Mlimani Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’, Abdallah Hemba amesema nao wataonesha umahiri mkubwa leo katika ukumbi huo na watawapa mashabiki wao wimbo unaotamba sasa unaoitwa ‘Jinamizi la Talaka’ ambayo ni albamu yao mpya iliyo na vibao vinane. Nyimbo ambazo zitakumbukwa leo ni pamoja na Kasimu wa Kustarehe, Selina, Huba, Talaka Rejea, Tui la Nazi na kadhalika.

Abdallah Hemba ambaye ni muimbaji ataongoza jahazi la Sikinde leo Dar Live huku wakiwemo wapiga magitaa mahiri, Mjusi Shemboza, Kaingilila Maufi , Tony Bass na Ally Jamwaka. Hassan Rehani Bitchuka anayefahamika zaidi kwa jina la Super Stereo atafanya vitu adimu. Kama hiyo haitoshi, atakuwepo pia Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa na bendi nzima ya Tanzania One Theatre (TOT) kukamilisha burudani hiyo ya Valentine’s.

Twanga Pepeta chini ya mwana mama Luiza Mbutu akishirikiana na ‘Kamarada’ Ally Choki nao pia wataonesha umahiri wao usiku wa leo ambapo watapiga nyimbo zao za zamani zilizowapatia umaarufu. Baadhi ya nyimbo hizo ni Kisa Cha Mpemba, Fainali Uzeeni, Mtu Pesa, Safari 2005, Aminata, Busu la mwaka 2000 na nyinginezo.

Bendi hiyo inayotamba kwa staili ya Kisigino pia itapiga nyimbo zao kama Nyumbani ni Nyumbani, Dunia Daraja,‘Mwana Dar es Salaam’, ‘Shida ni Darasa’, ‘Rafi ki Adui’, ‘Mwisho wa Ubaya ni Aibu’, ‘Nazi Haivunji Jiwe’, ‘Sitaki Tena’ na ‘Ganda la Miwa”.
Bendi hiyo itawajumuisha wanamuziki wake mahiri kama Kalala Junior, Saleh Kupaza na wengine wengi. Ukikosa usiku wa leo, umekosa raha.

NGWIJI wa Muziki wa Dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ amesema wanamuziki wawili mahiri nchini, Linex na Christian Bella wapo juu kutokana na uwezo wao wa kuimba.
Akizungumza katika kipindi maalum cha Mboni Show hivi karibuni, King Kiki alisema: “Kwa kweli vijana hao wanaweza, wanatunga na kuimba vizuri sana muziki.”


Loading...

Toa comment