The House of Favourite Newspapers

Kenya kuamua juu ya sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja

 

MAHAKAMA ya Kenya  leo itatoa uamuzi kuhusu uhalali wa sheria inayoharamisha mapenzi kwa watu wa jinsia moja. Chini ya sheria za Kenya, mapenzi ya jinsia moja ni hatia iliyo na hukumu ya miaka 14 gerezani.

 

Kenya, kama ilivyo katika mataifa mengi barani Afrika, uhusiano wa jinsia moja haukubaliki kwa jamii. Brian na Yvonne ni wanaharakati wa kutetea haki za jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, pamoja na wale waliojibadilisha jinsia na hisia.

 

”Tunadharuliwa, tunakabiliwa na ghasia, tunaumia, tunateswa, tunakosewa. Tukienda kutafuta huduma za afya tunaangaliwa kwa dharau, tunatukanwa, tunatemewa mate, tunafanywa kama sisi si Wakenya, kama sisi si binaadamu, ni kama sisi ni viumbe wasiotoka katika dunia hii,” alisema Yvonne.

 

Chini ya sheria za Kenya zilizoandikwa enzi za ukoloni, mapenzi ya jinsia moja yametambuliwa kama kitendo kisicho cha kawaida, na kuwekwa katika kitengo kimoja na hatia ya kufanya mapenzi na wanyama.

 

Wanaharakati wanasema kwamba kuwepo kwa sheria hii kumezidisha ubaguzi, huku watu wakifurushwa kutoka nyumba walizokodisha, kunyimwa nafasi za kupata matibabu na pia kuhangaishwa na polisi, yote kwa sababu ya jinsia zao.

 

Aidha wanaharakati wanasema kutoelewa sheria hii kumechangia dhuluma za aina nyingi.

 

”Mtu anasema, hata Kenya hairuhusiwi, sheria inapinga, kwa sababu si watu wengi wanaokwenda kwenye hicho kifungu cha sheria kuelewa inasema nini. Yeye amesikia tu sheria, inasema,” amefafanua Yvonne.

 

“Kwa hivyo inawasukuma watu kuendelea kuwachukulia na kuwafanyia watu wa jamii hii vitendo vibaya. Kwa sababu kuna hii fikra kwamba sheria imesema.  Sasa ndiyo maana tumekwenda kortini hiyo sheria iondolewe kwanza, ndiyo tuweze kuongea,” ameongeza mwanaharakati huyo.

 

Katiba ya Kenya inaonya dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia. Wasemaji wa jamii hii wanahoji kuwa hata kama sheria hii haitaondosha kabisa ubaguzi, angalau wana matumaini ya kuwa itawanyang’anya polisi nguvu za kuwakamata kiholela.

 

Lakini wanaounga mkono sheria hii, yakiwemo makundi ya dini, wanasema kuwa kuondolewa kwa sheria hii huenda kukatoa fursa ya kuhalalisha ndoa kwa watu wa jinsia moja, ambayo kwa sasa haitambuliki kwenye katiba.

 

Mnamo 2016, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu liligundua kwamba wapenzi wengi wa jinsia moja wanaoishi nchini Kenya wanakabiliwa na ‘wasiwasi wa usalama kila siku’. Kumekuwepo na shinikizo kutoka mataifa mengi duniani kwa taifa la Kenya kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.

 

Lakini, Wakenya wengi, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, wanasema kuwa taifa hili lina matatizo makubwa zaidi ya kushughulikiwa na yanayopaswa kupewa kipaumbele.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.