The House of Favourite Newspapers

Kenya: Upinzani Watishia Kususia Uchaguzi Mkuu

0

 

KENYA: Mzozo mpya umeibuka kati ya tume huru ya uchaguzi nchini Kenya, na vinara wa mrengo wa upinzani wa NASA kuhusu utangazaji wa matokeo rasmi ya kura za Urais.

IEBC imeijibu mrengo wa upinzani wa Nasa kufuatia vitisho vyake vya kususia uchaguzi iwapo tume hiyo itafaulu kwenye rufaa iliyowasilisha mahakamani dhidi ya uamuzi wa mahakama ulioruhusu matokeo ya kura za Urais kutangazwa katika kituo cha kupigia kura.

Hii ni baada ya viongozi wa upinzani kuishauri IEBC dhidi ya kusaka njia za kubadili mipango hiyo ili kutangaza matokeo ya kura za Urais katika kituo cha kitaifa jinsi ilivyokuwa matokeo ya miaka iliyopita.

Tume hiyo kupita mwenyekiti wake Wafula Chebukati, imeeleza kuwa haitobadili msimamo wake wa kukata rufaa na kuwaambia viongozi wa upinzani kuheshimu mahakama na kutumia njia za kisheria kutatua malalamiko yao.

Viongozi wa mrengo wa upinzani wakiongozwa na Mgombea wa Urais, Raila Odinga, walitishia kususia uchaguzi iwapo tume hiyo itakata rufaa na kuruhusu matokeo ya Urais kutoka kila kituo kutangzwa kitaifa.

”Kuitishia IEBC kuhusu uamuzi wake wa kukata rufaa, ni kutishia uhuru wake, na wasioridishwa na hatua hiyo, wajiunge kwenye kesi wasake suluhisho za kisheria,” alisema Chebukati.

Taifa la Kenya linatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu wa Urais baadaye mwaka huu huku ushindani mkali ukitarajiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta anayewania kiti hicho kupitia mrengo wake wa Jubilee na Raila Odinga, anayebeba bendera ya mrengo wa Upinzani wa Nasa.

Takriban wagombea kumi na wanane wa Urais wamejitokeza.

Chanzo: BBC

 
Leave A Reply