Kenya Yakabiliana Na Mlipuko Wa Ugonjwa Usiojulikana Katika Jimbo La Kisii
Wizara ya Afya nchini Kenya imetangaza kuwa, imo mbioni kupambana na mlipuko wa ugonjwa usiojulikana ambao umeathiri zaidi ya watu 200 katika vijiji vitatu vya jimbo la Kisii eneo la Nyanza Magharibi ya nchi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mary Muthoni anasema kuwa, tayari maafisa wa serikali kwa ushirikiano na serikali ya jimbo la Kisii wamefika katika maeneo yaliyoathiriwa kuchukua sampuli za vipimo zitakazofanyiwa uchunguzi kwa minajili ya kujua chanzo cha maradhi hayo.
Aidha amesema matokeo ya uchunguzi wa maabara yatatolewa leo Jumanne. Dalili za ugonjwa huo usiojulikana ni pamoja na kuhara damu, kutapika, homa kali na maumivu makali ya kichwa.
Wakaazi walioathiriwa ni wa vijiji vya Nyamarondo, Nyarigiro, Nyabigege vinavyopatikana eneo la Mugirango Kusini.
Vituo vya afya eneo hilo tayari vimeripoti kushindwa kudhibiti idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika kutafuta matibabu ya ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza eneo hilo karibu wiki tatu zilizopita.
Hivi sasa idadi kubwa ya wagonjwa imelazimisha wengi kutumia kitanda kimoja na baadhi yao wamepelekwa katika jimbo jirani la Migori kwa matibabu.