The House of Favourite Newspapers

KENYATTA AZINDUA SARAFU MPYA KENYA, HAZINA PICHA ZA MARAIS

 

RAIS Uhuru Kenyatta leo Jumanne, Desemba 11, 2018 ameliongoza taifa kuzindua sarafu mpya za Kenya za thamani za Sh 1, Sh 5, Sh 10 na Sh 20, zilizozingatia  vigezo vya Katiba ya sasa ya nchi hiyo iliyozinduliwa mwaka 2010, ambazo zimeanza kutumika rasmi leo.

 

Akizungumza wakati wa shughuli hii iliyofanyika katika makao makuu ya Benki Kuu nchini (CBK), jijini Nairobi, Kenyatta amesema sarafu hizo hazitakuwa na picha za marais wa Kenya yaani marehemu Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki, bali zitakuwa na nembo ya maliasili na tamaduni zinazoitambulisha Kenya kulingana na katiba.

Sarafu ya Sh1 itakuwa na picha ya twiga, Sh5 nembo ya kifaru. Katiba pia inaeleza kwamba sarafu ya Sh10 inapaswa kuwa na picha ya simba na Sh20 ya ndovu, yote yakiwa maliasili ambayo Kenya inavunia kuwa nayo na kuvutia watalii.

 

Sarafu ya Sh1 itakuwa na uzito wa gramu 5.5 na rangi ya silver, Sh5 itakuwa na gramu 3.75 na kipenyo cha 19.5mm, Sh10 itakuwa na gramu 5, kipenyo cha 23mm na rangi ya njano nje, wakati ndani ikiwa na rangi ya silver. Sh20 itakuwa na gramu 9, kipenyo cha 26mm. Silver nje na njano ndani.

 

“Huu ni mwanzo wa Kenya kuzaliwa tena na ufanisi wake. Haya yote yanaonesha juhudi tunazojivunia kupitia katiba yetu na malengo ya Ruwaza ya 2030,” amesema Rais wa Kenya.

 

Kiongozi wa nchi ameeleza kufurahishwa kwake na juhudi za Benki Kuu ya Kenya kuzingatia maoni ya wananchi katika kuzipa sarafu taswira ya raslimali “tunazojivunia kama taifa”.

 

Uchanya

Amesema sarafu hizi mpya mbali na kuzingatia maliasili, zitaweza kutambuliwa na walemavu wakiwemo vipofu.

 

“CBK imekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha taifa linaafikia Ruwaza ya 2030 pamoja na kulitambulisha duniani,” ameeleza.

Rais aidha, ametumia jukwaa la uzinduzi wa sarafu hizi kuhimiza benki kutumia mifumo mipya ya ubunifu katika kufadhili na kupiga jeki biashara ndogo ndogo na zile za wastani (SMEs). Sekta ya SME, maarufu kama Juakali, imebuni nafasi za kazi kwa zaidi ya asilimia 75 ya Wakenya.

 

“SMEs mbali na kuchangia serikali ushuru, kupiga jeki benki, imebuni nafasi nyingi za kazi na kutuletea mapato mazuri,” amesema.

 

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na waziri wa Fedha Henry Rotich na Gavana wa CBK Profesa Patrick Njoroge. Rais Kenyatta amepokea hundi ya Sh800 milioni kutoka kwa CBK kwa niaba ya serikali.

 

Comments are closed.