The House of Favourite Newspapers

Kenyatta Mgeni Rasmi Sherehe za Uhuru TZ

0

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuanza ziara rasmi ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia kesho, Desemba 9 ambapo atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za uhuru wa Tanzania Bara zitakazofanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatano Desemba 8, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu amesema Rais Kenyatta atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uhuru kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan alioutoa Mei 2021 alipofanya ziara nchini Kenya.

 

“Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta kufanya ziara rasmi hapa Tanzania. Amekuja mara kadhaa kikazi lakini hakuwahi kufanya ziara rasmi. Kwa hiyo, ziara hiyo itaanza kesho kwa kushiriki katika sherehe za uhuru,” amesema.

 

Siku ya pili ya ziara yake, Balozi Kazungu amesema Rais Kenyatta na Rais Samia watashuhudia utiaji saini wa mikataba minane ya makubaliano ambayo itahusisha masuala mbalimbali.

 

Amesema Rais Kenyatta ataambatana na ujumbe wa mawaziri watano ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Biashara na Viwanda, Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Afya na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Advertisement Balozi Kazungu amesema wakati wa ziara ya Rais Samia nchini Kenya, viongozi hao walikubaliana kutatua changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zikitatiza uhusiano baina na mataifa hayo.

 

Amesema walianza kutatua changamoto hizo na walibaini kero 64 katika uhusiano wa Kenya na Tanzania na katika kipindi cha miezi minne, wameweza kutatua kero 46.

 

“Kero 18 zilizobaki ni zile za kiutawala kwenye taasisi zetu kama vile KRA na TRA (Mamlaka za Mapato za Kenya na Tanzania). Hata hivyo, kero hizo zinaendelea kutatuliwa,” amesema Balozi Kazungu.

Leave A Reply