The House of Favourite Newspapers

Kerr akubali Yanga inatisha

0

kerr

KOCHA Mkuu wa Simba, Dylan Kerr.

Mohammed Mdose Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, ameshindwa kuficha na kuweka wazi kuwa kiwango kizuri wanachokionyesha Yanga kwa sasa, kinadhihirisha wazi kuwa, wao ndiyo mabingwa watetezi na wamejipanga kuutetea ubingwa wao, lakini akaapa kupambana nao ‘bampa to bampa’ mpaka mwisho wa ligi na kuahidi kushinda.

Yanga mpaka sasa ipo kileleni ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tano na kushinda zote ikiwemo ile iliyozikutanisha timu hizo na Simba kukubali kipigo cha mabao 2-0.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kerr alisema kuwa hawezi kuficha kusema kuwa, Yanga ipo kwenye kiwango kizuri kwa sasa na ina aina ya wachezaji wapambanaji ambao haitakuwa rahisi kukubali kuuachia ubingwa, hivyo timu yake inabidi ipambane kwa nguvu nyingi.

Alisema kuwa kila anapoiangalia Yanga ikiwa inacheza anagundua kuwa timu hiyo ina kikosi kizuri, hivyo inamfanya afikirie zaidi kupata mbinu mpya kila wakati ili aweze kuishinda katika kuwania ubingwa.

“Nilipotua nchini nilijua fika kuwa Yanga ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi kuu, watakuwa kwenye kiwango cha hali ya juu na ndiyo ninachokishuhudia kwa sasa.

“Wapo kwenye kiwango cha hali ya juu, lazima tukubali hivyo, lakini hiyo mimi haiwezi kunivunja moyo wa kuzidi kupambana na kuwa bingwa na nina uhakika nitaweza kushinda,” alisema Kerr.

Yanga hivi sasa ndiyo timu inayoongoza kwa kila kitu kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu. Ndiyo timu ambayo imefunga mabao mengi zaidi (13) na imefungwa mabao machache zaidi (bao moja tu).

Hii inaonyesha kuwa ina safu hatari zaidi ya ushambuliaji na safu hatari zaidi ya ulinzi. Ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 15, sawa na Azam.

Hata hivyo, Simba ya Kerr nayo inaonekana kuanza vyema ligi kuu, kwani ipo nyuma ya Yanga kwa pointi tatu tu. Hali hii inaonyesha ushindani utazidi kuwa mkubwa zaidi msimu huu.

Leave A Reply