The House of Favourite Newspapers

Kerr amchenjia Mavugo

0

kochaDylanKerr.jpg Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr .

Hans Mloli,

Dar es Salaam

WAKATI viongozi wa Simba wakiendelea na harakati za kumnasa Mrundi, Laudit Mavugo huku nako kocha wa timu hiyo, Muingereza, Dylan Kerr ameibuka na kutoa masharti mapya kwa straika huyo na kuhakikisha anayatimiza kama kweli anataka kuitumikia timu hiyo.

Katika suala hilo, Kerr ameeleza kuwa akiwa kama kocha mkuu lazima kila mchezaji anayetaka kusajiliwa amuone kwanza kabla hajasajiliwa, vinginevyo atakuwa ametua hapo bila baraka zake.

Kerr amesisitiza kwamba kwa kuwa hajawahi kumuona Mavugo anayeichezea Vital’O mahali popote hata kwa video zake, anataka kuhakikisha kiwango cha straika huyo kwa kumuona kwanza kabla ya taratibu nyingine kuchukua nafasi yake.

Simba imekuwa ikihaha kuinasa saini ya mshambuliaji huyo lakini imekuwa ngumu Vital’O kumuachia, angalau sasa inaonekana imekuwa nafuu baada ya taarifa za Mavugo kumaliza mkataba wake klabuni hapo hivi karibuni.

“Nimezisikia sifa za Mavugo, lakini sijawahi kumuona mahali popote pale, hata video zake sijawahi kuzinasa, ningependa kumuona kabla ya kusajiliwa ili niweze kujua kiwango chake na mimi nimfahamu na kupima vitu vingi kwa ajili ya kikosi.

“Unajua wapo mastraika ambao wana sifa nzuri huko wanakotoka lakini muda mwingine baada ya kumchukua inakuwa tofauti, kwa hiyo ni lazima pia nimuone kwanza (Mavugo) kabla ya kumsajili kuichezea Simba. Ligi ya Burundi ni tofauti na ya hapa.

“Kama nilivyosema, hicho ndiyo kitu muhimu kwangu, lakini kama itakuwa tofauti na atasajiliwa kabla ya mimi kumuona basi atakuwa amekuja bila ya mimi kumpitisha,” alisema Kerr.

Hata hivyo, Simba wamedhamiria kurekebisha kikosi chao kwenye nafasi ya straika kupitia usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa Novemba 15 kabla ya kufungwa Desemba 15, mwaka huu baada ya kutofurahishwa na utendaji kazi wa mastraika wao ndani ya mechi tisa za awali za Ligi Kuu Bara.

 

Leave A Reply