The House of Favourite Newspapers

Kesho Mapema… Okwi Atakuwa Simba

0

KLABU ya Simba, imetangaza rasmi kuwa, kesho Jumamosi itampokea straika wao wa zamani, Emmanuel Okwi, tayari kwa kumpa mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia timu hiyo.

 

Okwi, raia wa Uganda, ambaye aliwahi kuitumikia Simba kwa vipindi viwili tofauti, anajiunga tena na timu hiyo akitoke SC Villa ya nyumbani kwao ambayo alikuwa akiichezea mara baada ya kuachana na SonderjyskE ya Denmark.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, hivi karibuni alikuwa jijini Kampala, Uganda kwa shughuli zake binafsi ambapo alitumia mwanya huo kumalizana na Okwi.

 

Hans Poppe amesema: “Nilienda Kampala katika mkutano wa mambo tofauti na soka, nikiwa kule nikaona mtandaoni kuna picha inasambaa kwamba eti Okwi ameingia Dar, picha hiyo ilimuonyesha akiwa amevaa kofia, sasa wakati naiona ile picha nilikuwa karibu na Okwi, nikaona bora niwaumbue watu waongo, tukapiga picha, nikazituma.

 

“Sasa watu wakabadilisha mada, wakaanza kuzungumza kwamba tushamalizana naye wakati mimi nilitupia picha tu bila ya kuandika chochote.

 

“Lakini hata hivyo, nikiwa kule nimezungumza naye na tumekubaliana, hivyo atakuja hapa Jumamosi (kesho) kusaini mkataba wa miaka miwili, tumeamua kumrudisha Okwi kwa sababu ni mchezaji mzuri na mara kadhaa alikuwa akitupatia matokeo mazuri.

 

“Okwi ana uwezo wa kubadilisha matokeo muda wowote, tumekuwa tukimfuatilia tangu awe anacheza soka Uganda na tumeona bado ni mchezaji mzuri, kitendo cha kufunga mabao saba kwenye mechi saba kimedhihirisha hilo.”

 

Said Ally na Omary Mdose
Leave A Reply