Mahakama Kuu imesikiliza sababu za Halima Mdee na wenzake 18 za kuomba ridhaa ya kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku Mawakili wa pande zote wakivutana kwa hoja ndani ya chumba cha Mahakama.
Aidha katika usikilizwaji wa maombi hayo, Serikali imeunga mkono maombi ya kina Mdee ya ridhaa ya kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama.
Katika usikilizwaji huo Mawakili wa Mdee na wenzake wametoa hoja mbalimbali mbele ya Jaji Mustapha Ismail juu ya kuomba ridhaa hiyo.
Katika hoja zao Mawakili wa kina Mdee wamebainisha hoja tano ikiwemo waombaji hao kuonyesha kuwa na maslahi, muda muafaka wa kufungua maombi hayo, kuonyesha hatua zilizochukuluwa kutafuta haki zinazoombwa kabla ya kwenda mahakamani na kubainisha mdaawa anayelalamikiwa.
Wakili wa Mdee na wenzake, Ipilinga Panya ameieleza mahakama kuwa katika maombi hayo wateja wao kupitia viapo vyao na maelezo yaliyoambatanishwa katika hati ya maombi wamekidhi vigezo hivyo vyote.
Baada ya mawakili wa Halima Mdee na wenzake kumaliza kuwasilisha hoja za kuomba ridhaa ya kufungua kesi kupinga wabunge hao kuvuliwa uanachama wa Chadema, mawakili wa chama hicho nao wakazijibu hoja hizo.
Wakili upande wa chadema, Peter Kibatala ambaye alikubali kuwa kina Mdee wana maslahi na haki ya kuja mahakamani, lakini alipinga kuwa maombi yao yamefunguliwa nje ya muda.
Kwa upande wake Kiongozi wa jopo la Makili wa Serikali wanaowakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (wajibu maonbi), Stanley Kalokola amesema kuwa waombaji hao wametimiza vigezo vya kisheria vya kupata ridhaa hiyo.
Amevitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na muda wa kufungua maombi, baada ya uamuzi wanaotaka kuupinga akisema kwamba wamefungu maombi hayo ndani ya muda kwani maombi yanapaswa kufunguliwa ndani ya miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi unaopingwa kwani uamuzi unaopingwa ni wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 wakati maombi yamefunguliwa Juni 23, 2022.
Baada ya pande zote mbili kuwasilisha hoja zao Jaji akaahirisha shauri hilo hadi Julai 06,2022 kwa ajili ya kutolea uamuzi wa hoja zotezilizoibuliwa.