The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Dkt. Slaa, Mahakama ya Kisutu Yasema Imefungwa Mikono Kuendelea Nayo…

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema imefungwa mikono kusikiliza kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt.Wilbroad Slaa kwa kuwa upande wa Serikali umekata rufaa mbili katika Mahakama ya Rufaa.

Hayo yameelezwa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati mahakama ilipotoa wito wa kuitisha shauri hilo baina ya upande wa Jamhuri na Utetezi, licha ya kwamba shauri hilo lilipangwa kuitishwa Februari 6, 2025.

Hata hivyo, licha ya mahakama kutoa wito huo mshtakiwa ambaye ni Dkt.Slaa hakuwepo mahakamani hapo kutokana na changamoto ya usafiri wa kutoka gerezani hadi mahakamani.

Hatua ya upande wa Serikali kukata rufaa ni kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Januari 30, 2025 ambayo ilitoa amri ya kwamba shauri hilo lirudi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili liendelee.

Itakumbukwa kwamba upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Madeleka uliwasilisha hoja Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya marejeo ya kesi iliyopo Kisutu kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka na dhamana ya Dkt.Slaa.

Kwa mara ya kwanza Dkt. Slaa alifikishwa mahakamani hapo  January 10, 2025 akikabiliwa na shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa X (zamani Twitter) katika kesi ya Jinai namba 993 ya mwaka 2025.