The House of Favourite Newspapers

Kesi ya kupinga sheria ya mtandao yaanza

0

cyber1

Kwa ufupi

Kesi hiyo namba 32 ya mwaka 2015 ilifunguliwa wiki iliyopita na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), kwa kushirikiana na mashirika mengine ya haki za binadamu, kikiwemo Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia kwa wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole.

By James Magai, Mwananchi

Dar es Salaam. Mchakato wa usikilizwaji wa kesi ya  Sheria ya Makosa ya Uhalifu wa Kimtandao umeanza, huku Mahakama Kuu  nchini ikiipa Serikali siku 14 kuwasilisha mahakamani hapo majibu yake ya  utetezi kuhusiana na kesi hiyo.

Kesi hiyo namba 32 ya mwaka 2015 ilifunguliwa wiki iliyopita na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), kwa kushirikiana na mashirika mengine ya haki za binadamu, kikiwemo Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia kwa wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole.

Leo kesi hiyo ilianza kutajwa mahakamani hapo, ikiwa ni hatua za awali za mchakato wa kuanza usikilizwaji wake, huku mahakama ikiiamuru serikali hadi kufikia Septemba 18, iwe imewasilisha majibu yake ya utetezi.

Amri hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Profesa John Ruhangisa, baada ya Serikali kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Richard Kilanga kuomba muda wa siku 14 kuwasilisha majibu hayo.

Pia  Jaji Ruhangisa kwa niaba ya majaji wenzake, Lugano Mwandambo na Winfrida Koroso, alitoa amri kwa upande wa mdai, kuwasilisha majibu ya ziada ya utetezi wa Serikali, ndani ya siku saba, zitakazo anza siku Serikali itakapokuwa imewasilisha majibu yake.

Upande wa mdai jana uliwakilishwa na Wakili Benedict Ishabakati, pamoja na Wakili Kambole mwenyewe ambaye pia ndiye mdai.

Jaji Ruhangisa alisema kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Oktoba 22, 2015, mchana, kwa ajili ya kupanga namna ya kuendesha usikilizaji wa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo mdai anapinga baadhi ya vifungu  vya  sheria hiyo akidai kuwa  vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na kwamba utekelezaji wake utakiuka haki mbalimbali za binadamu.

CHANZO: MWANANCHI

Leave A Reply