The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Lissu Yapigwa Kalenda Tena

LISSU

Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, leo imeshindwa kusikilizwa kwa mara nyingine kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu na kupigwa kalenda hadi Februari 14, 2017.

Akisoma maelezo ya kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa,  mwendesha mashtaka wa serikali aliiambia mahakama kwamba shahidi wa jamhuri aliyepaswa kuwasilisha ushahidi wake leo dhidi ya mbunge huyo ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema, amepata dharura ya kikazi.

lissu

Baada ya kuridhishwa na maelezo hayo, hakimu Mwambapa aliiahirisha kesi hiyo ambayo inatarajiwa kusikilizwa tena, Februari 14.

Lissu anakabiliwa na mashtaka ya kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Juni 28, 2016.

Wakati huohuo, kesi nyingine inayomkabili Lissu, wahariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapishaji wa gazeti hilo, Ismail Mahbood ambayo leo ilifikishwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, imeahirishwa hadi kesho, Januari 19, 2017.

Kwa mujibu wa wakili wa serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba, aliomba kesi hiyo isikilizwe siku nyingine kutokana na  kutokamilika kwa maelezo ya awali ya kesi hiyo.

Denis Mtima/ GPL

Comments are closed.