The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Mbowe, Wenzake: Ushahidi wa Video Kutolewa Mahakamani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeridhia kuonyeshwa video inayodaiwa kubeba matukio yanayomhusisha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe na wenzake wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni mwaka 2018.

 

Kwenye kesi hiyo ya uchochezi, awali mahakama ilikubali kupokea video (tepu) hiyo, iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri kama moja ya vielelezo muhimu kwenye kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018, hata hivyo upande wa utetezi ulipinga.

 

Uamuzi wa kuonyesha video hiyo umetolewa leo tarehe 19 Agosti 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya kupitia hoja za upande wa mashtaka na utetezi.

 

Video hiyo inayosemekana ilirekodiwa wakati wa ufungaji wa kampeni za uchaguzi mdogo  wa ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chadema Februari 16 mwaka 2018, inadaiwa kubeba matukio yanayomuonyesha Mbowe na wenzake tisa wakiwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi huo, na kwamba ina uhusiano na kesi hiyo.

 

Awali, upande wa mashitaka uliiomba mahakama hiyo kukubali kuonyesha video hiyo, huku upande wa utetezi ukipinga ombi la kuonyeshwa mahakamani hapo kwa kutumia vifaa vya nje.

 

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba ameeleza kwamba uamuzi huo unatokana na hoja pingamizi za upande wa utetezi zilitolewa na Wakili Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari na zile za upande wa Jamhuri zilizojibiwa na Wakili Paul Kadushi na Dk. Zainab Mango.

 

Hakimu Simba amesema, kamera hiyo na mkanda wa video zimeishapokelewa kama vielelezo mahakamani hapo kutoka kwa shahidi namba sita, Koplo Charles, aliyedai kwamba kamera hiyo ili ichezeshe picha ni lazima iingizwe vifaa vya nje.

“Pingamizi za picha za tukio zisionyeshwe mahakamani kwa kutumia vifaa vya nje, halina mashiko yoyote,” amesema Hakimu Simba.

 

“Kwa sababu hizo mahakama inaamuru hizo picha zionyeshwe mahakamani na Mahakama ya Kisutu ina vifaa vya vya Tehama vya kuonyesha video hizo,“ alisema.

Hakimu Simba ameaharisha shauri hilo kwa dakika ambapo amesema, mahakama ikirejea itakwenda kuonyeshwa video hiyo.

 

Kwenye kesi hiyo, viongozi tisa wa Chadema wanashitakiwa kwa madai ya uchochezi wa uasi na kufanya  maandamano bila kuwa na kibali, na kusababisha mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

 

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema–Taifa, Freeman Mbowe; Vincent Mashinji, Katibu Mkuu; John Mnyika, Naibu Katibu Chadema –Bara; Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu Zanzibar.

 

Pia wamo Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Comments are closed.