The House of Favourite Newspapers

KESI YA MBOWE YAPANGIWA HAKIMU MPYA, HUKUMU YA RUFAA FEB 18 – VIDEO

KESI namba 112/2018 inayowakabili baadhi ya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na wabunge wengine saba wa chama hico, imeendelea leo, Alhamis, Januari 31, kwa kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ambapo imepangiwa hakimu mpya, Kelvin Mhina.

 

Mahakama hiyo imeelezwa kuwa rufaa ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka dhidi ya Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko,  itaanza kusikilizwa  Februari 18, 2019  katika Mahakama ya Rufaa.

 

Akitoa taarifa hiyo mahakamani hapo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa alisema kwamba wanasubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa.

 

“Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuna rufaa iliyopo mahakama ya rufaa ambayo bado haijasikilizwa, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa, wakati tukisubiri maamuzi ya mahakama ya rufaa,” alisema Wankyo na kudai kuwa rufaa hiyo ya kupinga dhamana iliyokatwa na upande wa mashtaka itaanza kusikilizwa  Februari 18, 2019.

 

Naye wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari, akisaidiana na Hekima Mwasipu walikubaliana na hoja za upande wa mashtaka ambapo Hakimu Mhina baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 14, 2019 ambapo itatajwa tena.

 

Ikiwa ni mara ya kwanza tangu Mbowe na wenzake wafikishwe mahakama ya Kisutu, leo aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Singida Kaskazini kabla ya kuhamia Chadema, Lazaro Nyarandu, ameonekana mahakamani kufuatilia kesi hiyo.

Nyalandu ‘ALIVYOSHUHUDIA’ Mbowe Akirudishwa Segerea


Mbowe na Matiko wanaendelea kusota rumande kutokana na kufutiwa dhamana zao  Novemba 23, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri,  ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, kwa madai ya ya kukiuka masharti ya dhamana.

 

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vincent Mashinji; Katibu Mkuu Bara, John Mnyika; Katibu Mkuu Zaznibar, Salum Mwalimu; Wabunge Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Ester Bulaya (Bunda); John Heche (Tarime Vijijini) na Halima Mdee (Kawe).

 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

BREAKING | HALI YA MBOWE, MATIKO MAHAKAMANI LEO

Comments are closed.