testiingg
The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Shambulio la Mwili Kuendelea Kusikilizwa Mwezi Desemba 

0
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, inatarajia kuendelea kusikiliza kesi ya tuhuma za shambulio la mwili Desemba 7,2023 inayomkabili mfanyakazi wa Benki moja hapa nchini, Ibrahim Masahi ambae anatuhumiwa kumshambulia kwa nyundo jirani yake Deogratus Minja.
Inadaiwa kuwa Masahi alimshambulia kwa nyundo jirani yake huyo, baada ya Minja kwenda kumshitaki Serikali za Mitaa kwamba anatililisha maji machafu katika eneo lake.
Mahakama hiyo, ilipanga tarehe hiyo mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Amos Rweikiza, baada ya upande wa mashitaka kutokuwa na shahidi wa kuendelea kutoa ushahidi, kutokana na shahidi aliyetakiwa kupata udhuru.
Awali, Wakili wa Serikali, Salma Jafari amedai kuwa shahidi ambae alipangiwa kutoa ushahidi wake ni askari, ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu anasimamia mitihani ya kidato cha nne inayoendelea nchi nzima.
Amedai kuwa kwenye orodha yake shahidi aliyetakiwa kuwepo kwa ajili ya kuendelea kutoa ushahidi ni askari polisi mpelelezi, ambapo hakufika mahakamani kwa sababu anaesimamia mitihani ya kidato cha nne.
Baada ya wakili kudai hayo, Hakimu Rweikiza aliwaeleza upande wa mashitaka kwamba kesi hiyo inatakiwa kuendelea kusikilizwa kwa sababu inatakiwa kuisha mwezi wa tatu.
” Mshitakiwa dhamana yako inaendelea hadi Desemba 7,2023, upande wa mashitaka walete shahidi kesi iendelee kusikilizwa,” alisema Hakimu Rweikiza.
Masahi anatuhumiwa Januari 11, 2023 akiwa eneo la Mbezi Msakuzi ndani ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam alimpiga Deogratus Minja kwa nyundo na kumsababishia kupata madhara makubwa ya mwili mwake.
Katika ushahidi wake, Minja amedai kuwa tarehe hiyo saa mbili na nusu usiku  alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake Masahi, alimkuta kijana wa jirani huyo, baada ya kumuona alizungumza kwa kilugha kwa sauti kubwa ambae yeye hakuielewa.
“Ghafla kijana alikuja mbele yangu akanizuia nisipite, mara geti likafunguliwa akatoka Masahi akanihoji kwamba mimi ni kama nani na kwenda kumshitaki Serikali za Mitaa, sikumjibu chochote kijana wake akanipiga ngumi,”
“Nilimgeukia jirani yangu ili amuonye kijana wake, lakini na yeye aliinua shati lake akatoa nyundo akanipiga nayo kichwani baada ya kupata maumivu makali nilianza kukimbia huku nikipiga kelele za kuomba msaada,” amedai Minja.
Amedai kuwa, alianguka chini ndipo Masahi akaanza tena kumshambulia na nyundo mgongoni, maumivu yalipomzidi aligeuka, akampiga na nyundo kwenye mkono wa kulia na kwenye bega. Jirani mmoja alifungua geti na kumsaidia kwa sababu alikuwa ana kuja damu nyingi walimpeleka Hospitali ya Bochi kwa matibabu.
Leave A Reply