MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam inatarajia kuendelea kusikiliza kesi ya tuhuma za shambulio la mwili jumatatu inayomkabili mfanyakazi wa benki, Ibrahim Masah ambaye anatuhumiwa kumshambulia kwa nyundo jirani yake Deogratus Minja.
Aidha, inadaiwa kuwa Masah alimshambulia kwa nyundo jirani yake huyo, baada ya Minja kwenda kumshitaki Serikali za Mitaa kwamba anatililisha maji mchafu katika eneo lake.
Siku hiyo ilipangwa jana Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Amos Rweikiza, baada ya kutoa ahirisho fupi hadi Jumatatu kwa sababu muda ulikuwa umeisha, kwa hiyo asingeweza kusikiliza ushahidi wa shahidi wa pili ambae ni askari polisi.
“Hivi sasa ni 10:30 jioni tunaweza kweli kwenda na muda huu, au tupange ahirisho fupi ili tuendelee na usikilizwaji, naahirisha kesi hadi Desemba 12,12, 2023 saa tano asubuhi na siku hiyo upande wa mashitaka uje na mashahidi wawili,” amesema Hakimu Rweikiza
Kabla ya ahirisho hilo pande zote mbili zilidai kuwa wapo tayari kuendelea na usikilizwaji, lakini ilishindikana kwa sababu muda wa mahakama ulikuwa umekwisha na hiyo ilitokana na kwamba hakimu huyo alikuwa ana sikiliza ushahidi katika kesi zingine ambazo watuhumia wake wapo gerezani.
Awali, kesi hiyo iliahirishwa kwa sababu shahidi aliyetakiwa kutoa ushahidi wake, alikuwa anasimamia mitihani ya kidato cha nne inayoendelea nchi nzima.
“Kwenye orodha hapa shahidi aliyetakiwa kuwepo leo kwa ajili ya kuendelea kutoa ushahidi ni askari polisi mpelelezi, hajafika kwa sababu yupo anaesimamia mitihani ya kidato cha nne,” alidai Jafari.
Masahi anatuhumiwa Januari 11, 2023 akiwa eneo la Mbezi Msakuzi ndani ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam alimpiga Deogratus Minja kwa nyundo na kumsababishia kupata madhara makubwa ya mwili mwake.
Katika ushahidi wake, Minja alidai kuwa tarehe hiyo saa mbili na nusu usiku alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake Masahi, alimkuta kijana wa jirani huyo, baada ya kumuona alizungumza kwa kilugha kwa sauti kubwa ambae yeye hakuielewa.
“Ghafla kijana alikuja mbele yangu akanizuia nisipite, mara geti likafunguliwa akatoka Masahi akanihoji kwamba mimi ni kama nani na kwenda kumshitaki Serikali za Mitaa, sikumjibu chochote kijana wake akanipiga ngumi,”
“Nilimgeukia jirani yangu ili amuonye kijana wake, lakini na yeye aliinua shati lake akatoa nyundo akanipiga nayo kichwani baada ya kupata maumivu makali nilianza kukimbia huku nikipiga kelele za kuomba msaada,”alidai Minja.
Alidai kuwa, alianguka chini ndipo Masahi akaanza tena kumshambulia na nyundo mgongoni, maumivu yalipomzidi aligeuka, akampiga na nyundo kwenye mkono wa kulia na kwenye bega. Jirani mmoja alifungua geti na kumsaidia kwa sababu alikuwa ana kuja damu nyingi walimpeleka Hospitali ya Bochi kwa matibabu.
|