The House of Favourite Newspapers

Mawakili wa Lissu Wapinga Ucheleweshwaji wa Upelelezi wa Kesi ya Uhaini – Video

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa Jamhuri kukamilisha haraka upelelezi wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu. Hatua hiyo imekuja baada ya mawakili wa utetezi kuhoji ucheleweshwaji wa upelelezi huo ambao umekuwa ukiendelea chini ya Jeshi la Polisi.

Awali, upande wa Jamhuri uliomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo ili kutoa muda zaidi kwa polisi kukamilisha upelelezi.

Wakili Dk. Rugemaliza Nshala

Hata hivyo, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Dk. Rugemaliza Nshala, Mpale Mpoki na Peter Kibatala walipinga ombi hilo, wakitaka mahakama ipewe taarifa kuhusu kinachokwamisha upelelezi huo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga alikubaliana na mawakili wa utetezi kwamba hoja zao zina msingi, hasa ikizingatiwa kuwa kesi hiyo inagusa hisia za wengi. Hakimu Kiswaga aliahirisha shauri hilo hadi tarehe 2 Juni 2025, ambapo Tundu Lissu anatarajiwa kufikishwa mahakamani tena kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.