Kesi ya Uhujumu Uchumi Inayomkabili Manguruwe Kusikiliza Hoja za Awali

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia Novemba 18, 2025 kusikiliza hoja za awali katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya maarufu Dk.Manguruwe.
Usikilizwaji huo ulitarajiwa uwe leo Novemba 17, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki lakini umeshindikana baada ya Wakili wa Serikali, Titus Aron kusema kuwa Jamhuri bado haijakamilisha kupandisha nyaraka zote kwenye mtandao wa mahakama.
“Tunaomba tupangiwe tarehe fupi kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali’”.
Mbali na Mkondya, mshtakiwa mwingine ni Rweyemamu John (59) ambaye ni Mkaguzi wa Fedha wa Kampuni hiyo ambapo wanakabiliwa na mashtaka 28 ikiwemo kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Novemba 5, 2025 na kusomewa kesi ya Uhujumu Uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.
Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi 2020 na Disemba Mosi 2023 jijini Dar es Salaam walitenda makosa hayo.
Katika mashtaka 9 ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili
Mkondya peke yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

