The House of Favourite Newspapers

KESI YA VIDEO CHAFU… WEMA GIZANI SIKU 40

DAR ES SALAAM: Yupo gizani! Ndivyo unavyoweza kusema kuakisi mapito ya Miss Tanzania 2006/07, Wema Isaac Sepetu ambaye anaishi kwa wasiwasi, hofu na mawazo mengi ya kutojua hatma ya maisha yake kutokana na kukabiliwa na kesi ya kuchapisha na kusambaza maudhui ya ngono mtandaoni.  

 

Wema alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Novemba Mosi, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, ikiwa ni miezi michache nyuma tangu aepukane na msala wa madawa ya kulevya kwa kulipa faini ya shilingi milioni mbili.

 

NI SIKU 140 SASA

Tangu alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza kwa msala huo video chafu, hadi juzi Jumatano mrembo huyo atakuwa amehenyeka takriban siku 140 akitetewa na wakili wake, Reuben Simwanza. Kwa kipindi chote hicho, Wema amekuwa gizani kwa kutojua hatma yake.

KESI ILIVYOANZA

Oktoba, mwaka jana zilianza kuvuja picha za faragha za Wema kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha mrembo huyo akiwa na aliyekuwa mpenzi wake aliyefahamika kwa jina la PCK na ndipo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walipoanza kuchukua hatua.

 

Hatua ambazo walizichukua awali ilikuwa ni kwenda kumfugulia kesi katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama (Mabatini) jijini Dar ambapo jalada la kesi hiyo lilisomeka KJN/RB/13607/2018- KUCHAPISHA NA KUSAMBAZA MAUDHUI YA NGONO MTANDAONI.

 

APATA WAKATI MGUMU

Mara tu baada ya video hiyo chafu kuanza kusambaa, Wema alikuwa kwenye wakati mgumu kutokana na jinsi ambavyo alishambuliwa na Watanzania kwenye mitandao ya kijamii huku kila mmoja akimsema kwa lake.

 

Hali hiyo ilimlazimu mrembo huyo kujitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kuvuja kwa video hiyo huku akionesha kujutia kilichotokea na kueleza wazi kulisababishwa na ‘utoto’ wake.

 

“Kuenea kwa picha hizo kumetokana na upumbavu na utoto wangu, niwaahidi Watanzania kwamba hilo halitotokea tena naomba radhi kwenu wote,” alisema Wema akionesha kuumizwa na kukoseshwa raha na jambo hilo.

ABADILI MFUMO WA MAISHA

Kutokana na msala huo, Wema alilazimika kubadili mfumo wake wa maisha kwa kukaa mbali na wanaume ambapo alionekana kuwa karibu zaidi na familia yake ambao ndiyo walikuwa msaada pekee wa kumtia moyo ili aweze kuibeba fedheha kubwa iliyompata.

 

Tofauti na ilivyokuwa zamani kwamba Wema alikuwa amezoeleka kuwa mtu wa kujiachia sana kwenye viwanja vya starehe, Wema akawa mtu wa kushinda ndani na kama ni kutoka, basi ni mara mojamoja tena katika mambo yenye umuhimu tu.

 

KUPUNGUA

Ni wakati huohuo ambao Wema alipungua mwili hadi kuzua mshangao kwa mashabiki wake ambao walizoea kumuona katika muonekano wa unene wa wastani, ghafla alikuwa mwembamba hali ambayo baadhi ya watu waliitafsiri kuwa huenda kupungua huko kumesababishwa na mawazo juu ya kesi hiyo.

 

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti, mrembo huyo alikaririwa kwenye vyombo vya habari akieleza namna ambavyo anajutia sana nyenendo zake kwa wanaume hususan PCK ambaye alimsababishia matatizo hayo makubwa kwa jamii na kumharibia heshima yake.

 

Wema alikiri kuwa, kati ya mambo ambayo anayajutia kwa kiasi kikubwa maishani mwake ni pamoja na hilo la PCK ambalo limemfanya apunguze imani kwa wanaume na kujikuta akiishi bila ya kuwa na uhusiano kwa muda mrefu.

SAFARI ZA MAHAKAMANI

Novemba Mosi, Wema alifikiswa kwa mara ya kwanza kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar na kusomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mahira Kasonde ambapo alikana kosa hilo kisha kuachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 kupitia kwa Salim Limu.

 

Hakimu aliahirishwa kesi hiyo hadi Novemba 20, mwaka jana ambapo haikusikilizwa kwa sababu ilikuwa Sikukuu ya Maulid. Kesi hiyo iliendelea tena mahakamani hapo Novemba 21 ambapo iliahirishwa tena hadi Desemba 12.

 

Siku hiyo, shauri la kesi hiyo lilifika kwa ajili ya kutajwa mbele ya hakimu Maira Kasonde huku upande wa wakili wa utetezi akiwa Ruben Simwanza na upande wa Jamhuri ukisimamiwa na Wakili Jenifer Masue.

MWAKA HUU

Februari 22, mwaka huu, Wema alifika katika mahakama hiyo ambapo alikana kuchapisha video za ngono kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo kesi yake ilitarajiwa kuanza kusikilizwa Machi 18, 2019. Baada kusikilizwa Machi 18, kesi hiyo iliharishwa hadi Aprili 18, mwaka huu kwa ajili ya kutolewa hukumu

Comments are closed.