The House of Favourite Newspapers

KESI YA WAETHIOPIA 40 YAAHIRISHWA KISUTU

0

KESI ya raia 40 wa Ethiopia waliokuwa wanakwenda Afrika Kusini wakipitia Tanzania imeahirishwa leo hadi Oktoba 13 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Kesi hiyo ilikuwa imekuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

 

Watuhumiwa hao walikamatwa wakisafirishwa na madereva wa kampuni ya Dangote Cement inayomilikiwa na mfanyabiashara tajiri Afrika, Aliko Dangote. Watu hao ni Hussein Hassan na Juma Mtambo na Sadick ambao wiki iliyopita dhamana yao ilikuwa wazi.

 

Awali kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay, alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano ambayo ni kuingia nchini kinyume na sheria. Ilidaiwa Septemba 25 mwaka huu watuhumiwa walikutwa maeneo ya Mbagala-Kongowe, wakiishi bila kuwa na kibali.

 

Kosa jingine ni usafirishaji usio halali linalowakabili madereva Watanzania waliowasafirisha ambapo inadaiwa Septemba 20 mwaka huu, maeneo ya Mbagala, Kongowe, na Mtoni Mtongani walikutwa wakisafirisha Waethiopia hao kwa kutumia gari ambalo ni mali ya Dangote Cement kuelekea Afrika Kusini.

 

Baada ya kusomewa makosa hayo, raia hao wa Ethiopia walikiri makosa yao ambapo Watanzania walikana na Wakili Mlay alisema upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.

 

Hakimu Nongwa alisema washtakiwa waliokana makosa wanaweza kupata dhamana kwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu ambapo washtakiwa waliokiri kosa walitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

 

NA DENIS MTIMA/GPL

Leave A Reply