The House of Favourite Newspapers

Kessy atua kuivaa TP Mazembe, atoa kauli nzito kwa Simba

0

KESSY (3)

Beki mpya wa Yanga, Hassan Kessy.

Na Wilbert Molandi na Nicodemus Jonas

YANGA wameshatua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuivaa TP Mazembe katika mchezo wa Kombe la Shirikisho, lakini beki mpya wa Yanga, Hassan Kessy, ametoa kauli nzito maalum kwa klabu yake ya zamani ya Simba.

 

Kessy ambaye ameshasaini mkataba wa kuijiunga na Yanga licha ya kuwa mkataba wake na Simba ulikuwa umesaliwa na siku chache kumalizika, amesema:

 

“Simba ndiyo walianza kuvunja mkataba kati yangu na wao.” Mchezaji huyo yupo katika msuguano kutokana na kudaiwa kuwa Simba haijatoa barua ya kuthibitisha kumalizana na Kessy, hivyo mchezaji huyo anaweza kuwa katika hatihati ya kuukosa mchezo wa kesho dhidi ya TP Mazembe kwa kuwa kanuni zinataka mpaka klabu aliyotoka mchezaji kuthibitisha kwa barua kuwa wamemalizana na Kessy na hivyo kuwa huru kuichezea Yanga.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu mara baada ya kuwasili nchini usiku wa kuamkia jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Kessy ambaye mkataba wake na Simba ulitakiwa kumalizika Juni 30, 2016 alisema anashangaa Simba kumuwekea ‘kauzibe’ wakati hawajamlipa mshahara wake wa miezi miwili.

Kessy

“Nawashangaa sana wanavyoning’ang’ania, mbona mimi silalamiki kwa kutolipwa mshahara wangu wa Aprili na Mei. Kwa muda wote ninalipwa na Yanga, mbona sijawalalamikia wanipe mshahara maana kisheria wanatakiwa kunilipa, mbona mimi siongei? “Wao ndiyo wamekuwa wa kwanza kukiuka makubaliano ya kimkataba na tayari wameuvunja kwa msingi huo,” alisema Kessy.

 

Awali, Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alinukuliwa akisema tayari wameandika barua kwenda Simba wakiomba wapinzani wao hao waandike barua ya kuthibitisha kumalizana na Kessy lakini bado hawajapata majibu. Muro alithibitisha kuwa tayari wamepata kibali cha wachezaji wengine waliosajiliwa ambao ni Andrew Vicente, Juma Mahadh, Benno Kakolanya na Obrey Chirwa.

 

Wakati huohuo, Simba kupitia Ofisa Habari wake, Haji Manara ilitoa taarifa juu ya suala hilo la ambapo alisema hawajapokea barua yoyote kutoka Yanga kuhusu suala la Kessy na wala hakuna mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi wao na wale wa Yanga. Manara pia alisema kauli za Muro kuhusu mashabiki wa Yanga kukaa upande unaotumiwa na wale wa Simba kwenye

Uwanja wa Taifa ni za kuchochea vurugu, amedai kuwa klabu yake haimzuii shabiki wao kushabikia timu yoyote anayoitaka. Wakati Manara akisema hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema kuwa wao wapo tayari kuwaandikia Yanga barua ya Kessy lakini kama tu watawafuata kiungwana na siyo kwa majigambo kama ambavyo wamekuwa wakijitangaza.

 

“Wakija kiungwana tutawasikiliza na kumalizana nao lakini wakionyesha dharau watasubiri mpaka mkataba umalizike rasmi ndiyo wamtumie,” alisema Poppe. Aidha, TFF imesema kuwa inalaani kauli za baadhi ya wadau na viongozi wa Yanga za kuwashawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni katika mchezo huo. TFF imesema itachukua hatua kali wote watakaohusika na pia kufanya hivyo kunaweza kuathiri timu mwenyeji kutozwa faini na ikiwezekana kuondolewa mashindanoni.

 

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia akisaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos wa Angola na Berhe O’Michael wa Eritrea huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.

Leave A Reply