The House of Favourite Newspapers

Kessy Yanga…

0

Hassan-‘-Kessy’-Ramadhani.jpgBeki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy.

 

Wilbert Molandi,

Dar es Salaam

ZIMEBAKI siku 26 tu ili beki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy, awe huru kuzungumza na timu yoyote ile inayomhitaji kumsajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine.

Inamaana kwamba, baada ya siku 26, Kessy atakuwa amebakiza miezi sita tu katika mkataba wake na Simba na tayari taarifa zinasema Yanga imeanza kupiga ndogondogo ili kumnasa beki huyo mbishi.

Mbaya zaidi ni kwamba, Kessy ambaye yumo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichopo Afrika Kusini kujiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Algeria, amegoma kuzungumza na Simba kuhusu mkataba mpya.

Ukiachana na Yanga, timu nyingine iliyotajwa kumuwania Kessy ni Azam FC ambayo itashiriki msimu ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika. Beki huyo alitua kuichezea Simba kwenye usajili wa dirisha dogo msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar baada ya timu hiyo kumnunua kwa dau la shilingi milioni 35.

Yanga na Azam ndizo mara nyingi zimekuwa zikiibomoa Simba kwa kuwanyakua wachezaji wao ikiwemo hivi karibuni Azam ilimsajili kiungo mshambuliaji, Ramadhan Singano ‘Messi’ kwa dau la zaidi ya shilingi milioni 60.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba, beki huyo amegomea mazungumzo kati yake na viongozi wa timu hiyo wakimtaka aongeze mkataba wa kubaki klabuni hapo.

Chanzo hicho kilisema, beki huyo hadi kufikia Desemba mwaka huu atakuwa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine yoyote itakayomhitaji kutokana na kubakiza miezi sita tu kwenye mkataba wake.

Kiliongeza kuwa, kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu itakayomhitaji ambapo Yanga na Azam zimeanza kuinyemelea saini ya beki huyo.

“Kati ya wachezaji wanaotupa presha katika kipindi hiki, basi ni Kessy, mara kadhaa tumemfuata kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya kuongeza mkataba lakini amekuwa akikataa.

“Sasa tunashindwa kuelewa sababu ni nini! Hali hiyo inatupa hofu ya yeye kufanya mazungumzo na klabu nyingine ya hapa nchini, lakini kama uongozi tunaendelea kufanya jitihada za kumshawishi kuhakikisha anaongeza mkataba.

“Kama unavyojua hizi timu za Yanga na Azam zinapoona Simba ina mchezaji mzuri basi lazima zitalazimisha kumsainisha ili aende akaichezee timu yao,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa meneja wa mchezaji huyo, Athumani Tippo kuzungumzia suala hilo, alisema: “Siwezi kuzungumzia suala hilo kwa kipindi hiki, Kessy bado yupo kwenye mkataba.

“Hadi kufikia Desemba, mwaka huu ndiyo nitaweza kuzungumzia suala hili kutokana na hadi kufikia mwezi huo atakuwa amebakiza miezi sita, hivyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu itakayomhitaji.”

 

Leave A Reply