Kiba akimbiza kijiji
“KUPENDA ni vitendo si manenomaneno, leo nakupa kitengo kwa kufika malengo, umeziba mapengo, kwa upendoupendo! Bora wananzengo waanze vikao vya sendo-ff eeeh maa! “Maana we mrembo nakujuzaaa… mama nashukuru umekuza, chanda kama pete nitakutunza…na umeshanizimaa, ayoyoyooo love, ayoyoyooo my love, ayoyoyooo love, your love, dodo langu baby!”
Hii ni sehemu ya mashairi matamu kinoma ya ngoma iliyoteka hisia za wapenda burudani mwishoni mwa wiki iliyopita. Ni Ngoma ya Dodo kutoka kwa mkali wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ambayo video yake ilirekodiwa kwenye hoteli ya kifahari pale Bubu visiwani Zanzibar yapata wiki mbili zilizopita.
Mfalme Kiba amerudi! Ndivyo yanavyosomeka maoni kibao chini ya video ya ngoma hii kwenye Mtandao wa YouTube.
Ghafla tu mjini na mitandaoni, gumzo likawa Kiba na video vixen wa ngoma hiyo, Hamisa Mobeto. Kwa nini? Eti kwa sababu Mobeto ni mzazi mwenza wa hasimu wa Kiba kimuziki, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’. Mjadala ukawa mzito, eti kwa nini Kiba amtumie Mobeto, kwani hakuona mrembo mwingine wakati wamejaa tele?
Hatujakaa sawa, eti tukasikia kuwa, kitendo cha Kiba kuachia ngoma hiyo kilisababisha Diamond au Mondi ashindwe kumtambulisha msanii wake mpya, Zuchu. So zoezi hilo likafanyika kimyakimya bila mbwembwe kwa sababu Kiba alikuwa tayari ameteka vichwa vya habari vya mitandao ya kijamii.
Tuachane na hizo stori halafu pia tuachane na stori kwamba eti kuna mtu alichezea viewers (idadi ya watazamaji) wa video hii kwenye YouTube zikashuka kutoka milioni moja hadi laki saba. Muziki huu una fitna nyingi mno na kama hujui, unaweza using’amue chochote. Huku unaambiwa watu huviziana ile mbaya ili kupata trending na vichwa vya habari.
Kwenye kichupa hicho, Kiba anaonekana amevaa kama mfalme na Mobeto amevaa kama malkia na maeneo mengine kama bibi harusi.
Mara ya mwisho Kiba kuachia ngoma yake binafsi ilikuwa ni Novemba, mwaka jana alipoachia Mshumaa na kufanya poa, hivyo mashabiki wake walikuwa wamemmisi kinoma na kuanza kupiga kelele nyingi za kwa nini hatoi ngoma mpya?
Ndani ya saa kadhaa tangu ngoma hii iachiwe Aprili 8, mwaka huu, ilianza kukimbiza kijiji kilichokuwa kimejitwalia trending za YouTube huku mashabiki maelfu wakiisifia na kuikubali kazi hii kutoka kwa bosi huyu wa Lebo ya Kings Music.
Taarifa ikufikie kwamba, mbali na kupata zaidi ya watazamaji milioni moja ndani ya saa 24 kwenye YouTube, lakini ndiyo ngoma inayokamata namba moja kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kama Tanzania, Kenya na Uganda kwa wakati mmoja, jambo ambalo huwa ni nadra sana kutokea.
Trending maana yake ni pale ngoma ya msanii inapokuwa moto kwenye kurasa mbalimbali za kijamii, lakini kubwa zaidi kushika namba moja kwenye YouTube.
Hicho ndicho kilichotokea kwa Dodo ya Kiba ndani ya saa 24 ambapo ngoma zote zilizokuwa zikipishana namba moja, zilijikuta zikipigwa ngeta ile mbaya kama ifuatavyo;
MISS BUZA-RAYVANNY FT DULLA MAKABILA
Ngoma ya Miss Buza ya Rayvanny na Dulla Makabila ilikuwa imeweka kambi kwenye namba moja, lakini saa tano tu zilitosha kwa Dodo kuipindua na kuitupa namba mbili. Hata hivyo, saa kadhaa tena, Miss Buza ilipigwa ngeta na Wana ya msanii mpya wa Wasafi, Zuchu ambaye alichukua namba mbili na Miss Buza ikajikuta ikiangukia namba tatu.
BEDROOM-HARMONIZE
Pamoja na kiki kubwa ya yule video vixen wake Nicole, lakini ngoma hii ilijikuta ikitupwa namba nne kutoka namba mbili kabla ya kupigwa tena ngeta na Bachela ya Queen Darleen na Lava Lava kutoka Lebo ya Wasafi ambayo ilikwenda namba nne na Bedroom ikaangukia namba tano.
BACHELA-QUEEN DARLEEN FT LAVA LAVA
Ngoma hii ilikuwa ikipanda kwa spidi ya ajabu, lakini ilikutana na kigingi cha Dodo, hivyo ikaishia namba nne huku ikiaminika kuwa ni vigumu mno kuiondoa Dodo pale kwenye namba moja.
TAMBA-MBOSSO
Pamoja na Ngoma ya Tamba kukaa kwenye namba moja kwa muda mrefu kabla ya kuondolewa na Miss Buza, lakini kishindo cha Dodo kiliifanya kutoka kabisa nje ya kumi bora na kujikuta ikisimama kwenye namba kumi na tano.
MAMA-HARMONIZE
Ngoma hii ilikuwa imepanda hadi kwenye kumi bora, lakini baada ya Dodo ilikimbizwa hadi namba thelathini.
NA NUSU -NANDY
Pamoja na kukaa kwenye trending kwa wiki nzima, lakini kishindo cha Dodo kiliifanya ngoma hii kutupwa nje kabisa ya ngoma zinazotrendi kunako YouTube.
NIONESHE-MAUA SAMA
Mkwaju huu mpya ulikuwa unapanda kwa kasi kubwa mno, lakini kitendo cha kuachiwa kwa Dodo, ngoma hii ilijikuta ikistaki kwenye namba tisa pamoja na kwamba mashabiki wa Maua Sama walikuwa wakilalamika kumisi ngoma mpya kutoka kwake. Swali linaloulizwa na wengi, je, ni nani wa kumjibu Mfalme Kiba? Tusubiri!
MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA



