The House of Favourite Newspapers

Kiba; Hili la Diamond sikufagilii mwanangu!

0

Kiba.jpgKWA mara nyingine, najaribu kuzungumza na msanii Ali Kiba kupitia safu hii, baada ya kukutana na maandishi yanayomnukuu akitoa kauli mbalimbali za kimuziki, hasa zinazoonesha ukubwa wa jina lake katika sanaa.

Ni kweli, Ali Kiba ni miongoni mwa majina makubwa ya vijana waliojipenyeza katika muziki wa kizazi kipya mwishoni mwa miaka ya 2000. Kila shabiki wa kweli anajua jinsi wimbo wake na hatimaye albamu yake ya Cinderella ilivyomtambulisha mwaka ule wa 2009.

diamond-platnumzBinafsi naukubali uwezo wake katika kuimba maana ni mmoja kati ya vipaji vya kujivunia ambavyo Bongo imewahi kupata katika Muziki wa Kizazi Kipya, akiwa kundi moja na wakali kama Q Chillah, Barnaba, Christian Bella na wengine wa aina hiyo.

Jambo moja ninalopingana naye mara zote ni jinsi anavyojaribu kwa nguvu kubwa, kukanusha uwepo wa bifu kati yake na Nasibu Abdul ‘Diamond’, lakini wakati huo huo akirusha vijembe vinavyoonesha kumlenga msanii huyo ambaye naye pia ni mwenyeji wa Kigoma.

Kwa wasanii, hasa wa hapa nyumbani, vijembe kwa wanaodhaniwa kuwa mahasimu wao ni vitu vya kawaida, lakini wanaojitambua zaidi, hukaa kimya na kupiga kazi, mwisho wa siku mashabiki wanakuwa ndiyo waamuzi wazuri.

Juzikati, Kiba aliandika sehemu jinsi msanii mmoja wa hapa nyumbani, anavyotumia fedha ili kushinda tuzo za kimataifa anazochukua kila siku. Huhitaji kuwa ‘genius’ kujua kuwa mlengwa ni Diamond. Kwamba tuzo alizotwaa hivi karibuni huko Nigeria, Afrika Kusini, Italia na Marekani ni za kununua.

Maana yake ni kubeza uwezo wa msanii mwenzake kwamba si lolote, hasa nikikumbuka huko nyuma aliwahi kusema yeye ni mkubwa kuliko tuzo. Siwezi kubishana na maoni yake, lakini nadhani siyo jambo baya kumshauri, hasa anapotoa maneno kwa wale ambao jamii inaamini ni maadui zake.

Kumbeza mtu ambaye kila siku anapata mafanikio kimuziki huku kila mmoja akimsifia, wakiwemo viongozi wakubwa serikalini, ni kuonesha ni kwa kiwango gani mtu una chuki, kitu ambacho siyo kizuri kisanii. Sikatai, King Kiba ni msanii mzuri, lakini Diamond kwa sasa ni levo nyingine.

Ninaongea na wasanii wakubwa ambao Kiba aliwakuta katika game, AY, FA, Profesa Jay na wengineo kadhaa, wanamkubali Diamond na wanamsifu kwa juhudi zake. Kwa Kiba kumsifu Diamond kwa mfano, hakumaanishi kuwa yeye ni dhaifu, bali inaonesha jinsi gani alivyopevuka katika hii fani.

Hivi msanii wa Afrika ana hela gani ya kwenda kuhonga Marekani au Italia, tena msanii huyo atoke Tanzania? Kuheshimu mafanikio ya mwenzako katika sanaa moja ni kichocheo kikubwa cha kuimarisha uwezo wako na wenye busara siku zote wanasema ukimya ni majibu mazuri sana kwa washindani.

Kuna wakati Profesa Jay aliwahi kuwa katika msuguano wa kimyakimya na Sugu, enzi hizo wote wakiwa mastaa ‘untouchable’ kwenye hili game, lakini kwa sababu kila mmoja anajua nini anataka na jamii inayomzunguka inavyomwelewa, hawa jamaa hawakuwahi kukwaruzana wala kutupiana vijembe kupitia media.

Kila mmoja kwa wakati wake, alipoombwa maoni kuhusu mwenzake, alimsifu kwa uwezo na mchango wake wa kutukuka katika muziki na hakukuwahi kuweko na sentensi inayoonesha kijembe, hadi leo wamekutana tena katika eneo lingine wakiendeleza harakati zao za miaka yote.

Ulimbukeni wa nani zaidi ndiyo uliowapoteza Dudubaya na Mr Nice, kwa sababu kama wangejua jinsi gani walivyoishika Bongo Fleva enzi zao, wangeweza kuitumia fursa na kutengeneza fedha nzuri.

Leave A Reply