The House of Favourite Newspapers

KIBA, JOTI WAMKOSHA RAIS MAGUFULI!

Nyumba ya kifahari ya Lucas Muhavile ‘Joti’.

 

Wakati baadhi ya wale wasiojituma wakidai ‘vyuma vimekaza’, wasanii; Lucas Muhavile ‘Joti’ na Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’ wameonekana kumfurahisha Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ kwani wameendana na dhana ya kujituma kwa jasho lao la kushusha mijengo ya ghorofa ya kifahari katika kipindi hikihiki kinachoonekana kigumu.

 

Rais Magufuli amekuwa akisisitiza katika ziara zake kuwa, wote wanaolalamika kuwa vyuma vimekaza ni wale waliokuwa wanapata fedha kwa njia zisizo halali, hivyo kama mtu anataka kufanikiwa, lazima afanye kazi halali.

 

MIJENGO YENYEWE

Licha ya wahusika kutotaka kuanika gharama za mijengo yao, Amani lilifanikiwa kufika kwenye mijengo hiyo na kuithaminisha ambapo kila mmoja umetajwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

Nyumba ya kifahari ya Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’.

TUANZE NA KIBA

Mjengo wa Kiba ambao upo Tabata-Segerea, maeneo ya Kwetu Pazuri, jijini Dar ni moja kati ya mijengo ya maana ambayo ni gumzo kubwa katika mitaa hiyo. “Unapozungumzia nyumba za kifahari zinazopatikana katika maeneo haya ya Tabata Segerea, kamwe huwezi kuiondoa nyumba ya Kiba.

 

Kwani sidhani kama kuna msanii wa Bongo Fleva anamfikia,” alisema Hussein Hilal, jirani wa Kiba na kuongeza: “Kwa kweli mjengo kama huu ambao umeanzia chini ya ardhi (basement) sidhani kama kuna msanii mwingine yeyote Bongo anao.”

Joti akiwa na mke wake.

Naye mmoja wa viongozi wa serikali ya mtaa wa Kwetu Pazuri akizungumza kwa sharti la kutotaja jina lake, alisema: “Kiba anaweza kuwa ni mmoja wa wasanii ambao wamemfurahisha zaidi mheshimiwa rais kutokana na kufanya kazi kwa bidii katika utawala wake huu, ambao baadhi ya watu wakiwemo wasanii wenzake hulalamika kila siku kuwa hali ni ngumu,” alisema kiongozi huyo wa mtaa.

 

Akizungumza na Amani, mmoja wa mameneja wa Kiba, Aidan Seif, alisema Kiba anajituma, anafanya shoo nyingi hivyo anastahili kuwa na mjengo kama huo. “We angalia shoo nyingi anazofanya Kiba nje na ndani ya nchi, anastahili kujenga zaidi ya mjengo ule mliouona,” alisema.

 

Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’.

JOTI SASA…

Aidha, kwa upande wake mchekeshaji Joti ambaye nyumba yake ipo maeneo ya Kibada, Kigamboni, naye amezua gumzo kubwa katika mitaa ya hiyo. “Wasanii aina ya Joti ndio watu ambao Rais Magufuli
anavutiwa nao, ukiangalia juhudi za msanii huyo unaona ana kila sababu ya kumiliki mjengo wa thamani kama huu. “We angalia Joti anavyojituma na kupata mashavu kibao ya matangazo, unategemea kama angekuwa si mtu wa kujishughulisha, angemiliki ghorofa la gharama kiasi hiki?” alihoji Ezekiel Kilala, fundi wa nyumba hiyo.

 

ZINAMALIZIWA MALIZIWA

Pamoja na nyumba hizo kuzua gumzo na kuwa na ubora na thamani kubwa lakini zote zipo kwenye hatua ya kufanyiwa ujenzi wa mwishomwisho (finishing).

 

YAWAACHA MIDOMO WAZI MASTAA

Chanzo kilicho karibu na mastaa wa muziki na filamu, kimeeleza kuwa mastaa wengi wamebaki midomo wazi baada ya kuiona mijengo hiyo. “Huwezi amini wapo mastaa wakubwa tu ambao wameanza gemu muda mrefu wamepigwa na butwaa baada ya kuona mijengo ya wasanii hawa, ni fundisho kwao na wanatakiwa kupambana waweze na wao kufikia hatua hii. “Waache kulalamika tu ooh, vyuma
vimekaza, vinakazaje wakati wenzao sasa hivi wanafurahia mijengo yao mipya wanayoikamilisha katika kipindi hikihiki kigumu?,” kilihoji chanzo hicho ambacho kipo karibu na mastaa.

 

WAMETOKA MBALI!

 

Kiba ana zaidi ya miaka 10 ndani ya gemu ya Bongo Fleva, amefanya shoo nyingi ndani na nje ya nchi hivyo kitendo cha muziki kumpa mafanikio hayo, kimeendana na uchapakazi wake. Uwezo wa Kiba ulianza kuonekana katika nyimbo zake za mwanzoni ikiwemo Cinderella, Nakshi Nakshi Mrembo na Macmuga kabla hajapotea kwa takriban miaka mitatu. Baadaye aliibuka na wimbo wa Mwana, ukafanya vizuri na kumweka juu ndani ya anga la Bongo Fleva ambapo aliendelea kuachia nyimbo nyingine kali ikiwemo Aje na hadi sasa, Seduce Me ambao unaendelea kufanya vizuri. JOTI Kwa upande wake Joti, amefanya uchekeshaji kwa zaidi ya miaka 10.

 

Alianzia mtaani, jina lake likakua zaidi alipokuwa akifanya Kipindi cha Orijino Komedi kilichokuwa kikirushwa East Africa Television na baadaye TBC1. Mbali na shoo yao kwenye televisheni kutoonekana kwa sasa, Joti amejiongeza na kuwa kivutio kwa kufanya matangazo mengi makubwa ambayo yanamuingizia kipato kikubwa hivyo hakuna shaka, anastahili kuishi katika mjengo huo wa gharama.

Stori: Ally Katalambula, Boniphace Ngumije na Mayasa Mariwata, Amani

Comments are closed.