The House of Favourite Newspapers

Kibabage: Nimekuja KMC Kupiga Kazi

0

KMC imefanikiwa kuinasa saini ya kiraka, Nickson Kibabage ambaye amekuwa akifanya poa akicheza beki wa kushoto na winga.

 

Kinda huyo amekuwa akiaminiwa na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, ambaye anauelewa uwezo wake tangu akiwa na kikosi cha Serengeti Boys mwaka 2017.

 

Moja kati ya kumbukumbu bora ni kwamba Kibabage ni zao la Serengeti Boys ambayo ilishiriki AFCON U17 mwaka 2017 nchini Gabon.

 

Kibabage ametua KMC akitokea kucheza soka nchini Morocco ambapo alikuwa akiichezea Difaa El Jadida.

 

Mwaka 2019, Kibabage alijiunga na Diffaa El Jadida ambayo 2020 ilimtoa kwa mkopo kwenda Youssofia Berrachid ambazo zote zinashiriki Ligi Kuu nchini Morocco.

 

Kinda huyo ambaye alizaliwa Oktoba 12, 2000, atatimiza miaka 21, aliwahi kuichezea Mtibwa Sugar kabla ya kwenda kucheza soka Morocco.

 

Spoti Xtra limefanya mahojiano naye na kufunguka mambo kadhaa.

 

UMEJISIKIAJE KUREJEA KUCHEZA TANZANIA?

 

“Najisikia vizuri kurudi nyumbani sehemu ambayo nimezaliwa na kujifunza mpira. Tanzania watu wanapenda sana mpira wa miguu na mimi nitajitahidi kuhakikisha nautendea haki katika Taifa langu.

 

IMEKUWAJE UMETUA KMC NA SIYO MTIBWA?

 

“Mtibwa Sugar ndio mara ya mwisho nilicheza pale kabla ya kutimkia Morocco, kila kitu ni mipango ya Mungu, naamini kama angependa mimi nijiunge na Mtibwa basi ningekuwa huko.

 

UMEJIPANGAJE KUCHEZA KIKOSI CHA KWANZA KMC?

 

“Hakuna mchezaji ambaye hapendi kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza, hata mimi napenda kuona hilo likitokea.

 

“Lakini kuhusu kuanza ndani ya KMC hiyo ni kazi mwalimu ambaye yeye ndiye atakuwa na mipango yake. Mwalimu ndiye kila kitu, kama akitaka nianze basi nitaanza, akitaka nianzie benchi itakuwa hivyo, akitaka nisicheze kabisa pia inawezekana.

 

UMEJIPANGAJE KUHAKIKISHA UNAFANYA VIZURI NDANI YA KMC?

 

“Ni kufanya mazoezi kwa bidii kubwa na kumuonesha mwalimu katika kiwanja cha mazoezi kuwa nipo tayari kwa ajili ya mechi na nahitaji kucheza.

 

“Kufuatisha maelekezo ya mwalimu kuwa anahitaji nini katika nafasi ambazo ananipanga ili niendane na matakwa yake, naamini kila kitu kitakuwa sawa.

 

UNAPENDA KUCHEZA NAFASI GANI?

 

“Popote ambapo nitapangwa na mwalimu nitacheza kwani naweza kucheza nafasi yoyote, sina sehemu maalum ambayo naipenda zaidi kati ya zile ninazozimudu ambazo ni beki wa kushoto na winga wa kushoto.

 

“Muhimu zaidi kwangu ni kucheza sehemu zenye matumizi ya kushoto, ukiangalia nilipokuwa Mtibwa Sugar nlikuwa natumika kama winga wa kushoto, nilipoenda Morocco nilitumika kama beki wa kushoto.

 

“Lakini Kocha wa Timu ya Taifa, Kim Poulsen hupenda kunitumia nicheze winga, hivyo popote nitacheza ambapo nitapangwa kwa kuwa sijajua Kocha wa KMC atakuwa ananitumia wapi zaidi.

 

UNA MPANGO WA KUCHEZA SIMBA AU YANGA?

 

“Mungu akijaalia itakuwa sawa kwa kuwa mpira ni kazi yangu, ila kwa sasa ningependa kuizungumzia zaidi KMC kwa sababu ndio timu ambayo naitumikia, na si nyingine.

 

MIPANGO YA KUCHEZA TENA SOKA NJE YA TANZANIA IPOJE?

 

“Hayo ndiyo malengo yangu makubwa, kurejea Tanzania sio kwamba haiwezekani tena kucheza nje ya nchi, sasa hivi ni kama najipanga upya kwa ajili ya safari ya kurudi huko nilipotoka.

 

“Bahati nzuri ligi ya Tanzania inafuatiliwa sana, hivyo matumaini yapo makubwa ya kupata timu nyingine, lakini hii inahitaji kupambana sana kwa kuhakikisha napata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili nioneshe uwezo wangu,” anasema Kibabage.

 

NA HAWA ABOUBAKHARI

Leave A Reply