The House of Favourite Newspapers

Kibabage: Ubaguzi wa Rangi Umeniondoa Morocco

0

NICKSON Kibabage ni moja wa wachezaji wachanga ambao wanakuja kwa kasi sana akiwa amefanikiwa kucheza nje ya nchi ukiachana na Ligi Kuu ya Tanzania.

Kibabage amefanikiwa kucheza katika timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu ya Morocco ambazo ni Difaa El Jadid na Youssofia Berrachid ambapo alicheza huko kwa mkopo akitokea El Jadid.

Ukiachana na timu hizo, pia Kibabage alifanikiwa kucheza katika Klabu ya Mtibwa Sugar, ambayo ndiyo ilimpeleka huko nchini Morocco.

Kwa sasa Kibabage yupo KMC ambapo amesajiliwa msimu huu akitokea nchini Morocco. Championi Ijumaa limefanikiwa kumtafuta Kibabage kufahamu changamoto gani zilizomkumba huko nchini Morocco na hajawahi kusimulia sehemu yeyote ambapo anafunguka kama ifuatavyo;

KITU GANI KIMEWAHI KUKUTOKEA HAKIJAWAHI KUANDIKWA WALA WEWE KUKISEMA?

“Ubaguzi wa rangi kwangu ndio tukio ambalo nadhani sikuwahi kulizungumzia katika maisha yangu ya mpira, kipindi ambacho nilikuwa nacheza mpira katika ligi ya nchini Morocco.

“Kule ubaguzi upo japo si mkubwa sana lakini upo wa chinichini, wachezaji wengi sana hukumbana nao japo huwa hawapendi kuweka wazi juu ya vitendo hivyo ambavyo si vya kiungwana.

UPANDE UPI ULIONYESHA UBAGUZI WA RANGI KIASI KIKUBWA?

“Pande zote zinahusika sana katika ubaguzi wa rangi japo wachezaji wenzangu sio wote waliokuwa wakionyesha vitendo hivyo, ni wachache sana ambao walikuwa wanaonyesha Jambo hilo, na walikuwa wanafikisha ujumbe kupitia utani kumbe ndio wanamaanisha.

“Kwa upande wa viongozi walikuwa wanaonyesha vitendo hivyo waziwazi, wao hawakuwa wakificha haswa pale ambapo nilikuwa nikiongea nao kwenye mambo ya muhimu kuhusu maendeleo yangu ndani ya timu.

“Mashabiki wa timu walikuwa wanaonyesha vitendo vya ubaguzi pale timu inapohitaji matokeo, halafu unajikuta umekosea ndani ya uwanja hapo ndio matusi ya kibaguzi hutokea.

“Na kwa upande wa mashabiki wa upinzani ukiwa unaonyesha kiwango kizuri kiasi cha kuwapa tabu, kila mara wanaanza kukutukana au kukuita majina au ishara za mambo ya ubaguzi wa rangi.

WAKATI MPO NA MSUVA DIFAA ALIKUWA HAPATWI NA VITENDO HIVYO?

“Msuva kwake ilikuwa ni kidogo labda kupitia utani wa wachezaji ambao walikuwa wanaonyesha vitendo hivyo kupitia utani, lakini kwa mashabiki wa Difaa El Jadid hawakuwa wakimfanyia kwa kuwa alikuwa ndiye staa wa timu.

“Kwa upande wa mashabiki wa upinzani walikuwa wanaonyesha vitendo hivyo waziwazi, ili kumfanya auchukie mchezo husika lakini bado aliendelea kufanya vizuri.

UBAGUZI UMEKUATHIRI KWA KIASI GANI?

“Unajua haya mambo sio mageni kwenye mpira, lakini ni mageni kwenye mpira wa Tanzania na ndio maana inahitaji uwe na saikolojia nzuri kuendana nayo au kuyakabili pindi yanapotokea.

“Kuna wachezaji wengine hususa kabisa kuendelea na mechi baada ya kufanyiwa vitendo hivyo, na kwa kweli huwa vinaumiza sana haswa kwa wachezaji wa kigeni.

USHAWAHI KUFANYIWA UBAGUZI MECHI IKIENDELEA?

“Ndio imeshawahi kutokea na ilikuwa kipindi cha pili na hii ilitokea mara baada ya kutoa pasi ya bao la pili, baada ya hapo mashabiki wa upinzani wakaanza kuongea maneno ya kibaguzi kwa nguvu.

“Kama unavyojua mimi nacheza pembeni beki wa kushoto mara nyingi anakuwa karibu na mashabiki, hivyo nilikua nawasikia mara kwa mara, ilifikia hatua nilikua nashindwa kujizuia nikataka kususa kuendelea na mechi.

“Kilichonibakiza uwanjani niliona refa alikuwa anaandaa muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kukamilika, lakini kama ingekuwa mapema basi nisingeendelea na mechi.

KUHUSU WAMOROCCO WEUSI WAO HAWABAGULIWI?

“Wale ambao wana viwango vikubwa mpaka wanacheza timu ya taifa ya Morocco hawapatwi sana na vitendo hivyo, ila kwa wale wenye viwango vya kawaida ndio hupatwa na vitendo hivi.

“Lakini hili suala mpaka likutokee mwenyewe ndio inakuwa rahisi kufahamu, ila inakuwa ngumu kuelewa kwa mwenzako kwa kuwa kuna vitendo vingine vinafanyika kisiri sana.

UBAGUZI WA RANGI NDIYO CHANZO CHA WEWE KUONDOKA MOROCCO?

“Ndio, ni sababu kubwa ya mimi kuondoka huko, ubaguzi ulizidi nikashindwa kuvumilia, lakini sipendi sana kuongelea hili suala kwa kuwa sasa hivi naweka nguvu zangu kwa timu yangu mpya ya KMC.”

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply