The House of Favourite Newspapers

Kibu Denis Apata Uraia wa Tanzania

0

 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Kibu Denis Prosper alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini amekuwepo nchini Tanzania tangu mwaka 1998, akiwa na umri wa miaka sita, baada ya wazazi wake kukimbia machafuko ya kisiasa nchini humo.

 

Simbachawene amesema hayo akizungumzia uamuzi wa kumpa uraia wa Tanzania mshambuliaji huyo wa Simba SC na kuongeza kuwa amekuwa na nyaraka zinazoonesha ni raia wa Tanzania, ikiwemo kitambulisho cha uraia, kwani yeye alikuwa anajijua ni Mtanzania kutokana na kuingia nchini akiwa na umri mdogo, na hana historia yoyote na nchi yake ya asili zaidi ya kukulia Tanzania.

 

Amesema mshambuliaji huyo aliyejiunga na Simba akitokea Mbeya City ya jijini Mbeya amepewa uraia tangu Septemba 30 mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 (Rejeo la 2002), baada ya kupokea ombi lililopelekwa kwake na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Kibu Denis alivaa jezi ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Julai 13, 2021 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambao Tanzania iliibuka na ushindi wa magoli 2-0, huku mashabiki wakivutiwa sana na kiwango chake.

 

Leave A Reply