The House of Favourite Newspapers

Kichanga atelekezwa nje ya kanisa!

0

Stori: Chande Abdallah, Wikienda

Mbeya: Dunia haina huruma! Kichanga kinachokadiriwa kuwa na umri usiozidi miezi miwili, kimeokotwa jirani na Kanisa Katoliki Parokia ya Uyole kwenye Kijiji cha Hasanga, Mbeya baada ya kutelekezwa na mtu anayesadikiwa kuwa ni mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina la Asha Shafii.

Tukio hilo la kusikitisha lilijiri Februari 4, mwaka huu baada ya wakazi wa kijiji hicho kupita jirani na eneo hilo wakiendelea na shughuli zao na kukiona kichanga hicho kikiwa kimevishwa nguo vizuri na kuhifadhiwa kwenye kichochoro cha kuelekea kanisani.

Kwa mujibu wa wakazi wa Hasanga, mtoto huyo atakuwa ametelekezwa na mama yake baada ya kutokea kwa mgogoro kwenye familia yake kwa kuwa haonekani kutokea familia ya kimaskini.

“Huyu mama aliyemtupa atakuwa na mgogoro wa kifamilia maana mtoto mwenyewe amevalishwa vizuri, ana afya yake tena ni mzima kabisa, huyu atakuwa ametokea familia inayojiweza tu,” alisema mmoja wa wapita njia aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Joseph.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, mwenyekiti wa mtaa huo, Remy Mgaya alisema kuwa alipata taarifa za mtoto huyo kisha kwenda kumshuhudia.Alisema kwa sasa mtoto huyo amemkabidhi kwenye Dawati la Jinsia la Kituo cha Polisi Cha Uyole ambao wanaendelea na upelelezi ili kumpata mzazi wa mtoto huyo.

Mgaya aliongeza kuwa pembeni mwa mtoto huyo kulikutwa mkoba mdogo ambao ndani yake kulikuwa na nguo za mtoto na kadi ya kliniki iliyoonesha jina la mzazi kuwa ni Asha Shafii.

“Inasikitisha kwa kweli, ni mtoto mzuri wa kiume, mimi mwenyewe nilipomuona anacheka tu vizuri nilitamani awe wa kwangu, hili suala lipo mikononi mwa polisi na huyu mzazi atapatikana tu,” alisema mwenyekiti huyo.

Leave A Reply