The House of Favourite Newspapers

Kichanga Chaibwa Katika Mkasa Wa Kusikitisha

razak%25201%2520%2520-%2520mama%2520razakooooooooooooooo_002Mama wa mtoto, Mwalimu Dafina Matwika.

Akizungumza baba wa mtoto huyo, Salim Kombo, alisema Razak aliibwa Jumatano katika kituo cha basi cha Tabora ambako mama yake, Mwalimu Dafina Matwika, wa Shule ya Msingi Dirifu iliyopo Mpanda mkoani Katavi, alikuwa akisafiri naye kutoka Morogoro.

Akisimulia zaidi, Kombo elieleza kuwa mkewe (mama wa Razak), alikuwa akisafiri kutoka Morogoro alikokuwa mafunzoni katika Chuo cha Ualimu Morogoro, kuelekea katika kituo chake cha kazi, Katavi.

Alisema wizi dhidi ya kichanga hicho ulitokea alfajiri ya kuamkia Alhamisi wakati mkewe alipomwacha Razak mikononi mwa mdogo wake wa kike aliyekuwa ameongozana naye.

Tukio hilo limeshafikishwa katika Kituo cha Polisi Tabora na kufunguliwa jalada namba TAB/RB/7675/2016. Polisi wanaendelea pia kumtafuta mtoto huyo.

“Mke wangu (Mwalimu Dafina), alikuwa amekosa mahali pa kulala baada ya kufika Tabora saa 5:00 usiku na nyumba zote jirani za wageni kujaa.

Alazimika kwenda kulala katika ofisi ya basi moja na huko ndipo mama mwenye dera na mtandio alipomuiba mwanetu… hapa tumevurugwa. Polisi wanaendelea pia kumsaka na hivyo tunaomba yeyote atakayemuona atusaidie kufikisha taarifa, “ alisema Kombo.

Akieleza zaidi, Kombo alisema Razak ni mtoto wao wa pili.

“Inauma sana… hadi sasa hatuelewi huyo mama aliyemuiba ana dhamira gani kwa mwanetu. Tunaomba Watanzania wenzetu watusaidie kumpata,” alisema Kombo, akiongeza kuwa hivi sasa wamekuwa katika kipindi kigumu cha kutojua mahala alikopelekwa Razak.

ILIVYOKUWA KUIBWA KWA RAZAK
Akisimulia ilivyokuwa hadi mtoto Razak kuibwa, Kombo alisema chanzo cha yote ni Jumatano ya Oktoba 5, 2016, wakati Mama Razak (Mwalimu Matwika) alipoanza safari kutoka Morogoro alikomaliza masomo yake hivi karibuni kuelekea kwenye kituo cha kazi, Mpanda mkoani Rukwa.

Alisema safari hiyo ilimfikisha Tabora Mjini saa tano na nusu usiku. Alitafuta mahala pa kulala katika nyumba kadhaa za kulala wageni bila ya mafanikio baada ya zote kujaa na ndipo mwishowe alipolazimika kwenda kujihifadhi kwenye kituo cha basi mojawapo maarufu lililokuwa likisafiri kwenda Mpanda alfajiri ya siku hiyo.

“Ndani ya hiyo ofisi alimkuta mama wa makamo aliyevalia dera la rangi ya maziwa huku akiwa amejitanda ushungi. Yule mama alijitambulisha kwamba ametokea Dodoma anaelekea Mpanda… alipoulizwa na mama Razak mwenyeji wake ni nani huko Mpanda, mama huyo alijibu kuwa atamjua hukohuko kwa sababu ameambiwa akifika apige simu.

Baada ya hapo, yule mama akaanza kumsifia mtoto (Razak) kuwa ni mzuri na akataka akabidhiwe ili ambebe. Hata hivyo Mama Razak alikataa na kujibu kuwa atakaa naye mwenyewe,” alisema Kombo.

Alieleza zaidi, Kombo alisema kuwa baada ya hapo, wote wakalala pale huku mama Razak akiwa amemkumbatia mtoto wake.

“Ilipofika alfajiri, mama Razak aliamka na kumkabidhi binti aliyekuwa ameongozana naye amshike (Razak) ili yeye aende msalani.

Yule mama akataka aachiwe yeye mtoto, Mama Razak akakataa. Dakika chache baadaye akarudi na ndipo alipokuta kile kisichotarajiwa… alishangaa kumkuta binti aliyemuachia akiwa kama hajielewi, yule mama pia hakuwapo eneo hilo,” alisema Kombo na kuongeza:

“Hapo akashtuka. Alipomuuliza binti kwamba Razak yuko wapi, ndipo akamjibu kuwa hajui kwa sababu alimuacha na yule mama ambaye naye alishatoweka.”

Alisema mkewe alipomuuliza msichana kwamba ilikuwaje akamkabidhi Razak kwa huyo mama wasiyemjua, ndipo alipojibiwa kuwa yule mama aliyevaa dera alimtuma (msichana) aende akaangalie magari kujua kama yalishaanza kuondoka huku akimchukua mtoto na kubaki naye pale ofisini walikokuwa.

“Ni hapo ndipo alipoanza kulia na kupiga kelele kuomba msaada baada ya kujua kuwa Razak ameibwa. Yule mama alitafutwa eneo lote la jirabni hakupatikana. Baadaye taarifa zikafikishwa polisi… nao wanaendelea kujitahidi kadri wanavyoweza lakini hadi kufikia leo jioni (jana) bado alikuwa hajapatikana. Jambo hili limetuhuzunisha sana. Tunamuomba Mungu usiku na mchana (Razak) awe salama na mwishowe tumpate,” alisema Kombo.

Hakukuwa na taarifa zaidi za polisi kuhusiana na tukio hilo kufikia jana jioni. Hata hivyo, yeyote mwenye taarifa za mtoto huyo ameombwa kuzifikisha katika kituo chochote cha polisi au kupiga simu kupitia namba 0786 008324; 0745385861 na 0714008324.

CHANZO: NIPASHE

Comments are closed.