The House of Favourite Newspapers

Kiemba: Nimeamua Kuachana na Stand Baada ya…

0
Kiungo mkongwe wa Stand United ya Shinyanga, Amri Kiemba.

NA MUSA MATEJA  | CHAMPIONI IJUMAA | MAKALA

KIUNGO mkongwe wa Stand United ya Shinyanga, Amri Kiemba anatambulika katika soka la hapa nchini kutokana na ubora wake uwanjani uliodumu kwa miaka mingi.

Kiemba alijiunga na Stand United, misimu miwili iliyopita akitokea Simba, alitua hapo kutokana na kumvutia Kocha Patrick Liewig raia wa Ufaransa ambaye pia aliwahi kufanya naye kazi ndani ya Simba.

“Nimeamua rasmi kuachana na Stand baada ya kuona wamevunja mkataba wangu kwa kutonipa stahiki zangu zaidi ya miezi mitatu sasa jambo ambalo nimevumilia lakini sijaona hata dalili za wazi kutoka kwa viongozi kuonyesha nia ya malipo ya mishahara na posho kama ilivyo kwenye makubaliano ya mkataba wetu.

Amri Kiemba akiwa ndani ya jezi ya Stand United.

“Nilipenda sana kuitumikia Stand lakini tangu udhamini wa Acacia ulipovurugika wachezaji wengi tumekuwa tukiishi kwa wakati mgumu kiasi kwamba hali ya maisha yetu imekuwa ya kuungaunga,” hiyo ni kauli ya Kiemba alipoanza kuzungumza na gazeti hili.

Kiemba ambaye pia amewahi kuichezea Yanga, anasema: “Nimechoka kuendelea kuvumilia maana hata mishahara imekuwa shida kiasi cha kunifanya nishindwe kujikimu hadi kuwa tegemezi kwa familia yangu.

“Nimeamua kubaki Dar kwa kuwa sijaona tena thamani ya mpira, tangu wadhamini walipojitoa nimekuwa nikiomba fedha kutoka kwa mama watoto wangu jambo ambalo limeniumiza maana kutoa fedha kwenye miradi yangu ili nitumiwe wakati nilikuwa huko kwa ajili ya kuchuma niisadie familia, nimeona imetosha.

Kikosi cha timu ya Stand United.

“Bora nirudi nikae na familia yangu na hizo fedha ninazotumiwa zifanye mambo mengine.

“Najua kwa kiasi kikubwa soka la Bongo limekuwa na matatizo yanayofanana kama haya, hivyo ifikie muda watu wafahamu kuwa hata uvumilivu huwa una kiasi chake ukizidi sana mwisho wa siku unaweza kuwa dhambi maana utakuwa huishi kulalama juu ya stahiki zako ambazo ni halali kwa maana hiyo hakuna sababu ya kukifanya chako kikutese.”

MWISHO WA SOKA LAKE
“Hapa ndiyo nauona mwisho wangu wa kuendelea kucheza mpira, maana tangu nimeachana na Stand mwezi wa tatu mwaka huu baada ya kumaliza mechi yetu na Azam FC kule Chamazi na ligi kusimama kwa muda, niliendelea kushinikiza malipo yangu jambo ambalo halikuwezekana hadi leo hii ambapo unaona ligi inaelekea mwisho.

“Nipo nyumbani kwa muda na kubwa naangalia namna gani nitafuatilia haki yangu kupitia sheria na kanuni za soka baada ya hapo sitakuwa na mpango tena wa kujihusisha na mpira kwani nimekuwa nikicheza siku zote hizo kutokana na kukosa jambo mbadala la kufanya, lakini hata huku ambapo niliwekeza sehemu kubwa ya maisha yangu na nguvu nyingi naona hakufai hivyo nitafuatilia haki yangu kisha nitafanya mambo mengine kabisa.

“Natambua hadi sasa nipo huru, yaani hakuna mkataba unaonifunga kujiunga na klabu nyingine baada ya huu Stand kuuvunja kinyemela, ninachotazamia hasa kutoka moyoni ni kupumzika kabisa mambo haya na hata kama itatokea nikapata wazo au mtu akanishawishi nicheze tena basi siwezi kucheza zaidi ya misimu miwili kwenye ligi hii ya Bongo.

Vipi kuwa kocha?
“Hakuna jambo ambalo muda wote nikiwa mchezaji nimekuwa sikubaliani nalo kama hili la kuwa kocha baada ya kustaafu, sina mapenzi na kazi hii ya ukocha kwani natambua sana karaha zake ambazo kwa muda wote nilipokuwa nacheza nimekuwa karibu na makocha takribani wote na wamekuwa wakinieleza malalamiko yao pindi wanapozinguliwa na viongozi wa klabu hata wale wa timu za taifa.

“Pamoja na kwamba miongoni mwa makocha waliowahi kunifundisha wapo waliokuwa wakinitaka nijiendeleze kwenye fani hiyo, hayupo hata mmoja ambaye amewahi kunishawishi nikubali.

“Niko tofauti sana na wachezaji wenzangu maana hakuna hata siku moja ambayo nimelala nikaamka nikiwaza baada ya kustaafu nitafanya jambo lolote linalohusiana na michezo, nafikiri ndiyo sababu kubwa ambayo imekuwa ikinifanya nisimkubalie mtu alipojaribu kunishawishi kujikita tena kwenye mambo ya michezo.

“Hata kocha wa zamani wa Simba raia wa Uganda, Moses Basena, alinishauri nijiendeleze kwenye ukocha kwa kuwa mimi ni mwepesi wa kufuata maelekezo ya makocha na kila alichokifundisha, pia ilikuwa hivyo kwa Liewig, lakini wote niliwakatalia.

“Kuna baadhi ya wachezaji wenzangu nao wamekuwa wakinishauri hivyo, nakumbuka hata Liewig wakati najiunga na Stand alinitaka niwe nahodha kwa maana niwe namsaidia mambo hayo ya ukocha kwa wachezaji wenzangu lakini nilimkatalia kwani mimi huwa sipendi kuwa mtu wa kati.

“Aliyewahi kuwa Kocha wa Taifa Stars raia wa Uholanzi, Martin Nooij yeye alikuwa akinihubiria sana suala hili kiasi cha kufikia hatua ya kumwambia Malinzi anisaidie kujiendeleza na yeye akajitolea kunipeleka nchini kwao nikasomee kozi hiyo ya ukocha lakini nilimkatalia katakata kwani nimekuwa nikijiangalia umbo langu na jinsi nilivyo najiona sistahili kabisa kuwa mwalimu wa mpira.

Utafanya nini baada ya soka?
“Kuna ishu ambayo naiweka sawa kwa sasa na kama ‘itatiki’ basi sina mpango wa kujihusisha na mpira hivyo sitarajii kuonekana sehemu yoyote ile inayohusiana na mambo ya soka zaidi nitafanya mambo yangu na nitajidhatiti kwenye mambo yangu ya kifamilia maana sina ‘hobi’ hata ya kusema nitajihusisha na muziki wala mambo yoyote ya starehe.

“Mimi ni Muislamu safi ambaye ibada ndiyo sehemu kubwa ya maisha ninayopenda. Hili halina hata haja ya kutafuta mtu wa kuuliza ila utaona tu tangu nimeachana na Stand, mwezi wa tatu hadi leo wanaofahamu mimi nipo Dar, ni majirani na watu wa karibu maana wengi wao wanajua nipo Shinyanga na timu.

“Hiyo basi naomba ieleweke wazi kwamba uamuzi huu wa kuachana na mpira utaniwezesha kufanya shughuli zangu za kifamilia zaidi na kusimamia mambo ambayo yalikuwepo muda wote nikicheza,” anasema Kiemba.

Leave A Reply