The House of Favourite Newspapers

Kifafa cha mimba (Eclampsia)

pregnant-womanYapo matatizo mengi yanayowapata wanawake wajawazito na miongoni mwa matatizo hayo, ni kifafa cha mimba (Eclampsia). Ni hali ambayo huwatokea wajawazito kutokana na mvurugiko kwenye mfumo wa fahamu kuanzia kwenye ubongo ambapo mtu mwenye tatizo hili huwa na dalili kama za mtu mwenye kifafa cha kawaida, ikiwa ni pamoja na mwili kutingishika kwa nguvu kikipanda na kupoteza fahamu.

Kwa kawaida, kabla ya mtu kupatwa na kifafa cha mimba, huwa kuna kifafa cha awali kinachotokea ambacho kitaalamu huitwa Preeclampsia, ambacho kwa kawaida huanza kutokea ujauzito ukiwa na umri wa wiki ishirini, dalili kubwa ikiwa ni kuongezeka kwa presha ya damu (BP).

Kifafa cha mimba ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza katika kusababisha vifo vya akina mama wajawazito. Hakuna chanzo cha moja kwa moja kinachofahamika kuwa ndiyo kisababishi cha ugonjwa huo lakini kuna visababishi vingi ambavyo huchangia tatizo hili.

Baadhi ya visababishi hivyo ni pamoja na; kama ni mimba ya kwanza kwa mama, kama kuna historia ya Eclampsia kwa mama yako/ndugu yako, kama una chini ya miaka 20 au zaidi ya miaka 40 wakati wa ujauzito au kama ulikuwa na tatizo la High Blood Pressure kabla ya ujauzito.

Pia kama uzito wako ni mkubwa kulingana na urefu wako Overweight/Obesity, kama una historia ya Eclampsia katika mimba iliyopita, kama una mimba za mapacha,  kama ni mimba ya mapacha, ama baba wa ujauzito huo ni mpya kwa mama.

Dalili za tatizo hili, tukianzia na Pre-eclampsia, ni pamoja na mama mjamzito kuwa na presha ambayo ni kubwa kuliko kawaida! Hii huendana na dalili nyingine kama maumivu makali ya kichwa, kuvimba miguu, maumivu ya chembe moyo Epigastric Pain, kushindwa kuona vizuri Blurred Vision, mapigo ya mtoto kushuka na mtoto kutokukua vizuri tumboni Intra Uterine Growth Restriction.

Presha ikiendelea kupanda zaidi huweza kusababisha kondo la mtoto kuachia kabla ya muda, mtoto kufia tumboni, figo kufeli, seli chembe-sahani za mama kupungua (hizi ndiyo husaidia damu kuganda pale unapopata jeraha) na kusababisha mama kutoka damu sana na hata kufariki.

Kama presha ikiendelea kupanda, mama pia hupata degedege, kuanguka kifafa na pia kuchanganyikiwa akili au kupoteza fahamu.

Pre-eclampsia na Eclampsia hutokea mara nyingi kuanzia wiki ya 24, na pia baada ya kujifungua. Mara chache pia inaweza kutokea kabla ya wiki 24.

Hakuna matibabu ya moja kwa moja ya tatizo hili lakini kulingana na dalili za mama na wiki za ujauzito, madaktari wanaweza kujaribu kushusha presha yake kwa dawa na kumfanyia uangalizi wa karibu mpaka atakapojifungua.

Comments are closed.