The House of Favourite Newspapers

Kifo cha Mke wa Mzee Yusuf… Simanzi, Majonzi, Vilio na Huzuni!

0

DAR ES SALAAM: Simanzi! Habari yenye kuumiza moyo inamhusu aliyekuwa Mfalme wa Taarab Bongo na Mkurugenzi wa Bendi ya Jahazi Modern, Alhaj Mzee Yusuf kupata pigo kubwa la kufiwa na mkewe mdogo (wa pili), Chiku Khamis na kichanga chake.

 

Mmoja wa Wakurugenzi wa Jahazi na Meneja wa Ukumbi wa Dar Live, Juma Mbizo aliliambia Wikienda kuwa, Chiku alifariki dunia juzi, jioni katika Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu wa Ilala jijini Dar ya Amana, alikokuwa amepelekwa kwa ajili ya kujifungua ambapo mtoto naye hakuwa riziki.

MZEE YUSUF AFUNGUKA

Akizungumza na Wikienda, Mzee Yusuf aliyestaafu muziki na kuamua kumrudia na kumtumikia Mungu alisema kuwa, alimpeleka Chiku katika Hospitali ya Amana, usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita na kwa bahati mbaya, operesheni (upasuaji) iliyofanywa kutokana na matatizo ya uzazi, haikwenda salama hivyo akampoteza mkewe na mtoto wa kiume aliyezaliwa.

 

MZEE YUSUF ABAKI NA LEYLA

Mzee Yusuf ambaye amebaki na mke wa kwanza, mwimbaji wa Taarab, Malkia Leyla Rashid, yupo kwenye simanzi nzito ya kufiwa na mkewe huyo ambaye amemuachia watoto wawili wa kike.
Msiba huo uliwekwa nyumbani kwa familia ya Chiku, Mtaa wa Livingstone, Kariakoo jijini Dar na kusababisha jiji zima kulipuka kwa vilio.
Wikienda lilimshuhudia Mzee Yusuf akilia kwa uchungu na watoto wake hao.
Mzee Yusuf aliliambia Wikienda kuwa, watoto hao ndiyo faraja pekee aliyoachiwa na mkewe Chiku.
“Hata hivyo, tunamshukuru Allah maana yeye ndiye mpangaji wa kila jambo,” alisema Mzee Yusuf.

LEYLA AZIMIA NUSU SAA

Kwa upande wake, Malkia Leyla aliyeshiriki msiba wa mke mwenzake, Chiku na kukumbwa na simanzi kubwa iliyosababisha kuzimia kwa nusu saa.
Leyla aliwasili nyumbani kwenye msiba jana, majira ya saa 5:00 asubuhi na kujikuta akishindwa kuyazuia machozi. Hali ilikuwa ngumu zaidi kwa Leyla wakati mwili wa Chiku ulipowasili nyumbani hapo ambapo alilia kwa uchungu hadi akapoteza fahamu.
Leyla alizinduka baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na watu wake wa karibu ambao walimpepea na kumwagia maji.

JOKHA KASSIM NAYE

Naye mwimbaji wa Taarab, Jokha Kassim ambaye amezaa mtoto mmoja na Mzee Yusuf, alifika msibani hapo na kujikuta akiangua kilio mara tu baada ya kuwasili.
Jokha, mke wa zamani wa Mzee Yusuf, aliwasili msibani hapo saa 5:30 asubuhi akitokea Zanzibar ambako anaishi na mumewe wa sasa, Amin Salmin.

VILIO VYATAWA KARIAKOO

Mzee Yusuf aliwaongoza waombolezaji waliofurika ambapo aliubeba mwili wa mwanaye kuelekea Msikiti wa Manyema, Kariakoo ilipofanyika ibada ya kuwaombea marehemu hao.
Kitendo cha miili hiyo kupitishwa mbele ya umati wa waombolezaji, wengi walishindwa kuzuia vilio huku wengine wakipoteza fahamu.
Baada ya kuswali, msafara wa mazishi ulielekea Makaburi ya Kisutu ambapo Chiku alizikwa na mwanaye pembeni yake.

MZEE YUSUF AMTUKUZA MUNGU

Katika hali ya simanzi, baada ya kumzika Chiku na mwanaye, Mzee Yusuf alianza kushusha vifungu vya Quran tukufu akimtukuza Mungu kwa mtihani mkubwa alioupata.
Wakati akiendelea kumtukuza Mungu, Mzee Yusuf alishindwa kuvumilia na kuanza kulia, hali iliyosababisha kuondolewa makaburini hapo kwa msaada wa waombolezaji.

NENO LA MHARIRI

Wikienda linaungana na wote walioguswa na msiba huu mkubwa, kutoa pole kwa Mzee Yusuf, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi awape subira katika kipindi hiki kigumu. Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina! – Mhariri.

Stori: Richard Bukos | Ijumaa WIKIENDA

Kifo cha Mke wa Mzee Yusuf… Simanzi, Majonzi, Vilio na Huzuni!

Leave A Reply