BUKOBA: Utata! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya aliyekuwa mlinzi kwenye makampuni mbalimbali, Edward Rweyemamu Ngamera Mkazi wa Nyakanyasi, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera mwili wake kukutwa umenyongwa na kutupwa maeneo ya Bukoba Club Darajani karibu na Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa chanzo, marehemu alitoweka nyumbani kwake Nyakanyasi Jumamosi kuelekea kwenye mkutano wa mtaa ambao ulikuwa ukifanyika jirani na anapoishi.
“Marehemu (Edward) huwa ana kawaida ya kutumia bodaboda, mara nyingi anaye dereva wake ambaye anampeleka sehemu mbalimbali. Siku ya tukio alitoka bila kuwa na bodaboda wake kwa kuwa alikuwa akielekea katika mkutano jirani na nyumbani kwake.
“Alihudhuria vizuri mkutano na ulipomalizika majira ya jioni tulimshuhudia akichukua usafiri wa bodaboda hatukujua ni nani lakini hakuwa yule dereva wake tukajua anaelekea kwake, nashangaa hakurudi hadi tulipomkuta kesho yake ametupwa akiwa tayari ameshafariki dunia,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kinaeleza utata mwingine ni marehemu siku ya tukio alienda kwenye kikao akiwa na laini tu ya simu huku simu zake mbili akiwa ameziacha nyumbani. “Kawaida marehemu alikuwa akimiliki simu mbili lakini tunashangaa siku ya tukio alikutwa na laini tu jambo linalotuacha katika utata mkubwa,” chanzo kiliweka nukta.
Akizungumza na Amani, mtoto wa marehemu, Angela Edward alisema kuwa baba yake alimuaga anakwenda kwenye mkutano lakini siku ya Jumapili mchana walipelekewa taarifa na mzee wa kanisa kuwa kuna kitambulisho kimeokotwa kina picha ya baba yao pamoja na laini ya simu kwa hiyo inabidi kwenda kuhakiki mwili.
“Walimchukua mama na kwenda kuhakiki mwili na wakakuta ni mwenyewe. Baba alikuwa mtu wa watu, alikuwa mpole na si kwa watu wa nje, hata ndani alikuwa mkimya mpaka kujua shida au tatizo lake ni mpaka akwambie.
“Ilipofika majira ya saa nne usiku mama aliingia chumbani kwa ajili ya kuandaa nguo za kanisani kwa kuwa kesho yake ilikuwa Jumapili ndiyo akazikuta simu zipo juu ya redio tukashangaa iweje asahau na kwa nini ameacha zote mbili jambo ambalo si kawaida yake siku zote?
“Kuziangalia simu zote hazina laini, kuweka laini nyingine hakuna hata jina simu zote zinaonekana kama mpya yaani zimefutwa kila kitu,” alimaliza kusema Angela. Rafiki wa marehemu ambaye pia ni dereva wake wa bodaboda, Wilson Kabito aliliambia gazeti hili kuwa, marehemu alikuwa mtu wake wa karibu walioshirikiana katika mambo mbalimbali.
“Hadi sasa sijui hata kilichomsibu maana mara ya mwisho alikuwa vizuri kwa hiyo sijui ni majambazi au nini kimempata. Marehemu hakuwahi kugombana na mtu na wala sikuwahi kusikia neno baya kutoka kwa watu,” alisema Kabito. Kwa mujibu wa ripoti ya daktari inaonesha kuwa marehemu umekufa kwa kukabwa.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi aliomba kupewa muda kwa kuwa alikuwa mbali na mazingira ya ofisini. Mwili wa Edward ulitarajiwa kuzikwa jana, Nyakanyasi Bukoba.
Stori: Kutoka Gazeti la AMANI
Comments are closed.