Kigogo Yanga aivaa TFF, kisa kipigo

 

BAADA ya juzi Jumamosi kikosi cha Simba kukumbana na kipigo kikali kutoka kwa Al Ahly ya Misri katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mmoja kati ya viongozi wa Yanga amelivaa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Kiongozi huyo amedai kuwa TFF ndiyo inayopaswa kulaumiwa juu ya kipigo hicho kutokana na tabia yake ya kusogeza mbele mechi za Simba za Ligi Kuu Bara kila wakati ambazo ilitakiwa kucheza, kwa madai kuwa wanaipatia muda wa kujiandaa na mechi zake za kimataifa.

 

Katika mchezo huo juzi Simba ilitandikwa mabao 5-0 jambo ambalo liliwashitua vilivyo viongozi hao wa Yanga lakini pia wapenzi na mashabiki wa soka hapa nchini ikiwa ni muda mfupi tu kupita baada ya kupata kipigo kama hicho kutoka kwa AS Vita ya DR Congo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, kiongozi huyo ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema kuwa, TFF inapaswa kulaumiwa kwa hilo kutokana na tabia yake ya kusogeza mbele kila wakati mechi za Simba za ligi kuu kwa kile inachoona kuwa inaisaidia ili iweze kujiandaa na mechi zake za kimataifa, jambo ambalo siyo sawa.

 

Alisema Katika mechi mbili ambazo Simba imekutana na vipigo vikali, ilipocheza dhidi ya AS Vita lakini pia dhidi ya Al Ahly, wachezaji wa timu hiyo hawakuwa na ‘match fitness’.

 

“Hii inatokana na timu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuja kupumzika Tanzania wakisubiria mechi nyingine za michuano hiyo.

 

“Watu wanadhani Kuwa wanaisaidia Simba kwa kuwabadilishia ratiba yao ya ligi kuu, wakae wakijua kuwa wanaiharibia. Nikiwa kama mtaalamu wa mambo ya michezo na niliyebobea katika mchezo wa soka, hali hiyo ndiyo imesababisha wakumbane na vipigo hivyo.

 

“Wamekuwa wakicheza bila ya uelewano na kama wasipobadilika basi Simba katika kundi lake hilo ushindi pekee inaoweza kuupata ni ule iliyoshinda hapa nyumbani dhidi ya JS Saoura,” Alisema Tiboroha.

 

“Wakati Nilipokuwa Yanga tulikutana na Al Ahly mara mbili, mwaka 2014 na 2016, Katika mechi zote hizo hawakutusumbua hivi na kila tulipokutana nao uwanjani tuliwasumbua sana na kidogo tu tungewatupa nje ya michuano hiyo, kwa hiyo Simba wajipange kama wanataka wafanye vizuri katika mechi zijazo.”

 

Mwaka 2014, Yanga ilitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

 

Hatua hiyo ya penalti ilikuja baada ya Yanga kuifunga Al Ahly bao 1-0 hapa nchini na ilipoenda Misri nayo ikafungwa 1-0. Mwaka 2016, Yanga pia ilitupwa nje ya michuano hiyo na Ahly kwa jumla ya mabao 3-1, katika mchezo uliopigwa hapa nchini timu hizo zilitoka sare ya 1-1 na ziliporudiana huko Misri, Yanga ilifungwa mabao 2-1.

Sweetbert Lukonge, Dar es Ssalaam

Toa comment