The House of Favourite Newspapers

Kigwangala kuikarabati nyumba ya Nyerere

Waziri Kigwangalla akifanya ziara katika Makumbusho ya Kumbukizi ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere, Magomeni Mtaa wa Ifunda.

 

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla (MB) ambaye amefanya ziara ya kushitukiza katika Makumbusho ya Kumbukizi ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni Mtaa wa Ifunda namba 62, ambayo aliishi kabla ya uhuru, amesema wizara yake itaikarabati.

Dk. Kigwangalla aliyeitembelea nyumba hiyo hivi karibuni alijionea mambo mbalimbali ndani ya makumbusho hayo huku pia akipokea maoni ya namna ya kufanyiwa maboresho ya kituo hicho ikiwemo ufinyu wa eneo la ofisi na maegesho ya wageni wanaotembelea hapo.

 

…Akipewa maelekezo.

 

“Nimefika hapa leo kujionea kituo hiki ambacho ni kielelezo kikubwa cha mwasisi wa taifa letu. Hapa pana hazina kubwa na kituo hiki kina mambo mengi ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kwa hali tuliyoikuta kwa kweli tutakaa na timu yangu kuona tunafanya maboresho makubwa kabisa ili kiwe kama maeneo mengine yenye waasisi wa mataifa yao.

 

Nyumba ya Nyerere.

 

“Tumeona kama eneo alilozaliwa mzee Nelson Mandela kule Afrika Kusini, nyumba yake imehifadhiwa vizuri na imekuwa na wageni wengi,” alisema Dk Kigwangala.

Akaongeza: “Hapa tutajenga maktaba ambapo watu watakuja kusoma vitabu vya mwasisi wetu na kuona mambo aliyokuwa akifanya. Lakini pia tutaonana na viongozi wa Halmashauri ya Kinondoni kuona namna ya kupaboresha mahala hapa ikiwemo miundombinu ya barabara ya kuingia na kutoka eneo ili.”

 

Akipatiwa maelekezo.

 

Pia aliongeza kuwa, kituo hicho kipo katika hali mbaya kikikabiliwa na changamoto nyingi licha ya kuwa ni kituo muhimu sana hapa nchini na mipango iliyopo ni pamoja na kukifanyia marekebisho kutengeneza choo, kupaka rangi pamoja na kufanyia ukarabati mkubwa vionyeshe kumbukumbu nzima ya baba wa taifa.

Alisema lengo kwa sasa ni kuifanya nyumba hiyo iwe kama nyumba halisi alivyokuwa akiishi mwenyewe Baba wa Taifa kwani ndani bado kuna vitu halisi alivyokuwa akivitumia na mikakati ni pamoja na kununua hata nyumba za jirani ili kuongeza eneo na kuongezwa baadhi ya ofisi na pawe na hadhi kama mwasisi mwenyewe.

 

 

“Kiukweli nimefika hapa kushuhudia makumbusho haya ambayo kiuhalisia hapa ni hazina kubwa sana ya kumbukumbu ya taifa letu hasa katika harakati za kupigania uhuru pia zilianzia hapa katika nyumba hii.

 

“Pia tutaboresha zaidi kwa kuweka studio maalumu ambayo pia tutaboresha CD zote za Baba wa Taifa zitakuwa zikioneshwa humo ikiwemo zile za hotuba,” alisema.

Awali Muhifadhi Mkuu wa Makumbusho hayo, Neema Mbwana alieleza changamoto zinazoikabili kituo hicho pamoja na kuomba kuboreshwa kwa vitu muhimu ikiwemo ukarabati wa nyumba nzima, ikiwemo, paa na kupaka rangi.

Na Mwandishi Wetu

Comments are closed.