The House of Favourite Newspapers

 KIHARUSI; MAMBO MUHIMU YA KUYAFAHAMU

KIHARUSI ni ugonjwa wa dharura na hatari mno ambao hutokea pale seli za ubongo zinapokufa kwa kukosa hewa safi ya ya oksijeni na chakula kutokana na kuziba au kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo. Ni miongoni mwa magonjwa yanayosumbua sana kwa sasa ambayo siyo ya kuambukiza.

 

AINA ZA KIHARUSI

Kuna aina kuu mbili za kiharusi;

1: Kiharusi kinachotokana na kuziba kwa mishipa ya damu ya ubongo.

2: Kiharusi kinachotokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ya ubongo.

 

UKUBWA WA TATIZO LA KIHARUSI

1: KIHARUSI NI MUUAJI NAMBA MBILI

Kwa mujibu wa ripoti maalum ya Shirika la Afya Duniani (WHO), sababu za vifo vingi ilionesha kiharusi kinashika nafasi ya pili kati ya magonjwa yote kwa kusababisha vifo vingi.

2: KIHARUSI

HUSABABISHA ULEMAVU Kwa wengi kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiharusi kinashika nafasi ya tatu kati ya visabibishi vingi vya vya ulemavu duniani. Waathirika wengi wa kiharusi huishia kuwa walemavu.

 

DALILI ZA KIHARUSI

1: GANZI

Mtu anayepata kiharusi hupata ganzi inayoanza ghafla na mara nyingi huathiri upande mmoja wa mwili. Mfano; upande mmoja wa uso kufa ganzi na kushindwa kuongea vizuri au kutabasamu kama kawaida.

2: KUPATA SHIDA KUONGEA

Mgonjwa wa kiharusi hushindwa kuongea vizuri. Utoaji wa maneno huwa siyo wa kawaida.

Mfano; mgonjwa kushindwa kumaliza sentensi au kuongea kama amelewa sana.

Pia hali hii huweza kuambatana na kutoka mate (udenda) kwa wingi mdomoni.

 

3: KUSHINDWA KUONA

Mgonjwa wa kiharusi anaweza kushindwa kuona. Hali hii hutokea ghafla. Inaweza kuhusisha jicho moja au macho yote.

4: KUPOTEZA FAHAMU AU DEGEDEGE

Pia mgonjwa wa kiharusi anaweza kupoteza fahamu au kupata ugonjwa wa degedege.

5: KUSHINDWA KUZUIA HAJA

Mgonjwa wa kiharusi anaweza kushindwa kuzuia haja kubwa au ndogo au vyote viwili.

 

VITU VINAVYOCHANGIA MTU KUPATA KIHARUSI

1: Ugonjwa wa shinikizo kubwa la damu (presha).

2: Uvutaji sigara.

3: Ugonjwa wa kisukari.

4: Magonjwa ya moyo hasa ugonjwa wa mtetemo wa moyo (atrial fibrillation).

5: Tatizo la mafuta mengi kwenye damu (lehemu au cholesterol).

6: Uzito mkubwa uliopitiliza.

7: Unywaji wa pombe uliopitiliza au kukithiri.

8: Kutokufanya mazoezi ya mwili.

 

GUNDUA KIHARUSI HARAKA UOKOE MAISHA YA NDUGU, JAMAA AU RAFIKI

Kiharusi ni tatizo la dharura linaloweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kifo au ulemavu kama mtu asipopata matibabu mapema iwezekanavyo. Hivyo ni vyema kila mtu akafahamu dalili za kiharusi ili iwe rahisi kuzitambua na kuchukua hatua mapema mno.

Ili kurahisisha kumbukumbu za dalili za kiharusi kifupisho FAST (Face Arm Speech Time) hutumika kama ifuatavyo;

 

FACE (USO)

Angalia kama upande mmoja wa uso uko tofauti na mwingine. Mwambie mgonjwa anyanyue kope au akunje ndita au atabasamu. Upande ulioathrika utashindwa kufanya hivyo.

ARM (MKONO)

Mwambie mgonjwa anyanyue mikono kwa mbele au juu mara nyingi, mkono wa upande ulioathirika hushindwa kunyanyuka au hudondoka unaporudishwa chini.

 

SPEECH (UONGEAJI)

Mwambie mgonjwa wa kiharusi atamke jina lake. Mtu mwenye kiharusi hushindwa kuongea au huongea kama mlevi au hupata shida kutafuta maneno kama mtu aliyepoteza kumbukumbu.

TIME (MUDA)

Muda ni mali, chukua uamuzi wa kutafuta msaada wa kitabibu haraka maana kadiri unavyochelewa ndivyo kiharusi kinavyoharibu sehemu muhimu za ubongo.

Comments are closed.