The House of Favourite Newspapers

Kiiza, Ngoma ni tishio ligi kuu Bara

0

KIIZA-1

Mganda, Hamis Kiiza wa Simba.

Hans Mloli,Dar es Salaam
WAMETUMWA kazi! Ndivyo unavyoweza kuwaambia washambuliaji hawa wawili wa kimataifa, Mganda, Hamis Kiiza wa Simba na Mzimbabwe, Donald Ngoma wa Yanga ambapo licha ya kukimbizana kwenye ufungaji bora, wamekuwa na rekodi tishio zaidi msimu huu na kuwatetemesha waliowakuta.

Kiiza anashikilia usukani wa wafungaji bora kwa sasa kwa mabao yake matano lakini Ngoma yupo jirani kabisa kwa mabao yake manne, sawa na pacha wake, Mrundi, Amissi Tambwe hali inayowafanya vigogo wa timu hizo kutembea kifua mbele kwa kufanya usajili murua zaidi msimu huu kwa nyota hao.

Lakini utamu unakuja zaidi kwa kuvunja rekodi na nuksi walizotoa kwa timu hizo katika viwanja vya ugenini vilivyokuwa vigumu kwa Simba na Yanga kwa takriban misimu mitatu mfululizo na kuifanya njia ya kuchukua pointi tatu iwe nyepesi ugenini msimu huu.

Kiiza alikata kiu ya ushindi wa Simba waliyokuwa nayo kwa misimu mitatu mfululizo pale Mkwakwani, Tanga mbele ya Mgambo JKT kwa kufunga bao moja siku hiyo katika ushindi wa bao 1-0. Kabla ya hapo msimu uliopita Simba ilichapwa 2-0, kisha 2013/14, ikabonyezwa tena bao 1-0, kabla ya 2012/13 kukaziwa na kutoka suluhu ya 0-0.

Ngoma naye akajibu mapigo baada ya kutupia bao kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, Jumatano iliyopita ikiwa ni mara ya kwanza kuibuka kidedea baada ya kutulizwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa misimu mitatu mfululizo.

IMG_0352Awali 2012/13, Yanga ilibutuliwa 3-0, msimu uliofuata ikagongwa 2-0 lakini 2013/14 ikasuluhu kabla ya hivi karibuni kuona mwezi uwanjani hapo kwa msaada mkubwa wa Ngoma.

Lakini kingine kinachotisha kwa mastaa hawa ni kwamba kila mechi wanayocheza lazima watupie isipokuwa kwenye mechi moja tu iliyozikutanisha timu zao, ikiwa na maana mabeki wa timu nyingine zilizobaki inawawia vigumu kuwasimamisha mastaa hawa.

Kiiza alianza kutupia kwenye mechi yake ya kwanza dhidi African Sports kwa bao pekee katika ushindi wa 1-0. Kisha ikafuata ya Mgambo alipofunga moja kwenye ushindi wa 2-0, mechi iliyofuata walishinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar, akatupia hat-trick. Mechi yake ya mwisho ilikuwa dhidi ya Yanga waliyofungwa 2-0, baada ya hapo akaumia mazoezini na kukosa mchezo wa hivi karibuni walioshinda 1-0 dhidi ya Stand United.

Ngoma naye alishindwa kufunga katika mchezo wa Simba pekee, lakini ile siku ya kwanza, mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Coastal Union alifunga moja katika ushindi wa 2-0, walipoishindilia Prisons 3-0 naye akafunga moja, akafanya hivyo tena walipoitungua JKT Ruvu 4-1 kabla ya kukutana na Mtibwa.

Kama hilo halitoshi, bado Kiiza ana mchango mkubwa kwa mabao ya timu mpaka sasa, katika mabao saba yaliyofungwa na Simba, yeye amefunga matano, Ngoma yeye amefunga robo ya mabao ya Yanga tangu msimu uanze, katika 13 amefunga manne.

Leave A Reply