Kijana Abadili Jinsia Yake Nchini Kenya

 

MIAKA 29 iliyopita kijana aliyezaliwa na jinsia mbili nchini Kenya, Ruth Wangui, amebadili jinsia yake na sasa ni mwanamume anayefahamika kama Ryan Muiruri.

 

Ni mmojawapo wa watoto wengi wanaozaliwa duniani kila mwaka walio na umbo lisiloweza kufafanuliwa kuwa ni mwanamke au mwanamme.

 

Kulingana na Ryan, alipozaliwa, mamake na mkunga waliamua kumpatia jinsia ya kike kwani walimuona kuwa na maumbile ya mtoto msichana. Uamuzi ambao haukumpatia amani katika miaka iliyofuata.

 

Baadhi ya watu wanaozaliwa na jinsia mbili, wanataka kutofautishwa na wapenzi wa jinsia moja, kwani hali zao wanaeleza ni kuhusu jinsia wala sio sifa za uume au uke.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kuna aina 42 tofauti ya watu wenye jinsia mbili ulimwenguni. Japokuwa hakuna takwimu zilizokusanywa kuhusu hili, wataalamu wanasema kuwa, kwa kila watoto elfu 20 wanaozaliwa, mmoja ana jinsia mbili.

 

‘?imi sikujua kwamba niko tofauti na watoto wengine wa kike, niligundua hilo nilipokuwa na umri wa miaka mitano nilipokuwa nikicheza na wenzangu,” Ryan amesema.

 

“Nilikuwa nikicheza wa wenzangu na shangazi yangu ambaye tuko rika moja, na baada ya muda nilianza kupigana na mwenzangu hapo ndipo wakagundua kwamba mimi sio mtoto msichana kamili kama walivyodhania, walinivua nguo na hapo ndipo niliweza kubaini kwamba ni kweli mimi niko tofauti, niligundua niko na sehemu nyingine ambazo wasichana wengine hawana.” Ryan aliongezea.

 

Anaeleza kwamba watu wenye jinsia mbili hubaguliwa, wengi hukosa kueleweka, na mara nyingi hutizamwa kama watu wenye laana.

 

 

Ryan ambaye sasa ni mwanaharakati na muasisi wa chama cha watu wenye jinsia mbili, anasema hali hii ya kuwa na jinsia mbili iliathiri maisha yake.

 

“Nilikuwa sina raha na hata marafiki zangu walinifanyia utani wakisema mimi huwa sitabasamu, lakini ni kwa sababu sijakutana na kitu chochote ambacho kimenifurahisha maishani mwangu.

 

“Tangu kisa hicho cha watoto kugundua kwamba mimi sio msichana kamili walienda shuleni na kutangaza siri yangu. Wakati nilipokuwa ninakwenda haja watoto walikuwa wakinifuata kunitazama iwapo mimi hujisaidia kama mvulana au huchuchumaa kama msichana, na maisha shuleni yalizidi kuwa magumu sana kwangu,” anasema.

 

Anaeleza hayo yalimfanya kutoroka shuleni na hata kujificha msituni lakini baada ya muda hilo likagunduliwa. “Mamangu mzazi aligundua hilo kwani sikuwa naandika chochote katika vitabu vyangu.”

 

Mwaka wa 2004, ndipo aliianza safari ya kubadili jinsia yake kuwa mwanamme na anasema ulikuwa mwaka mgumu sana.

 

“Mahali nilipolelewa walizingatia dini sana, kwa sababu hata watoto wasichana hawakuruhusiwa kuvaa surualei ila magauni tu.

 

“Nilipopata muda wa kutoka nyumbani nilikuwa najifanya kijana na nikaanza kuvalia mavazi ya kak’angu mdogo lakini niliporudi nyumbani ilinibidi nivae gauni na kujifanya mimi ni msichana kwani hivyo ndivyo wanavyonitambua,” anaongeza kusimulia.

 

Ryan anakiri kwamba ni mtihani mkubwa na amewasihi wazazi iwapo watagundua kwamba wamejaliwa mtoto wenye utata au tofauti kidogo, ni vyema kutafuta ushauri kwa wakati muafaka na amewasihi wale ambao wana jinsia mbili kujitokeza watafute uhuru wa maisha yao.

Loading...

Toa comment